Washindi wa mwaka 2022 ni

TUZO YA KISWAHILI YA SAFAL-CORNELL YA FASIHI YA AFRIKA: 2022

 Utaratibu wa Kushiriki

 

Tunafurahi kuwajulisha utaratibu wa kushiriki katika mashindano ya Tuzo ya Kiswahili ya Safal-Cornell ya Fasihi ya Afrika yanayoingia mwaka wake wa saba. Tuzo hii, iliyoanzishwa mwaka wa 2014 na Dkt. Lizzy Attree (Short Story Day Afrika) na Dkt. Mukoma wa Ngugi (Chuo Kikuu cha Cornell, Marekani), ina madhumuni ya kuhimiza uandishi kwa lugha za Kiafrika, na kuhimiza sanaa ya tafsiri kutoka lugha za Kiafrika, baina ya lugha za Kiafrika, na kwa lugha za Kiafrika. Jina la Tuzo limebadilishwa ili lilingane na jina la kampuni-mama la wafadhili wetu wakuu, Safal Group Limited. Kwa hivyo, kuanzia mwaka huu wa 2022 jina litakuwa: Tuzo ya Kiswahili ya Safal-Cornell ya Fasihi ya Afrika.

Tuzo itatolewa kwa mswada bora ambao haujachapishwa katika tanzu za riwaya, ushairi, mkusanyo wa hadithi fupi, riwaya za picha na wasifu. Kuanzia mwaka huu na kuendelea, hatutapokea vitabu vilivyochapishwa miaka iliyopita. Jumla ya $15,000 (za Marekani) zitagawanywa ifuatavyo:

  • Mshindi wa Kwanza (riwaya)  – $5,000
  • Mshindi wa Kwanza (ushairi)  – $5,000
  • Mshindi wa Pili (katika utanzu wowote)  – $2,500
  • Mshindi wa Tatu (katika utanzu wowote) – $2,500

Miswada itakayoshinda itachapishwa vitabu na shirika la uchapishaji, Mkuki na Nyota (Tanzania). Na diwani bora itatafsiriwa kwa Kiingereza na kuchapishwa na Africa Poetry Book Fund. Sherehe ya kuwatuza washindi, itakayohudhuriwa na wote waliofuzu kuwa kwenye orodha fupi, itakuwa Afrika Mashariki.

Namna ya Kushiriki na Mwongozo

Tafadhali peleka mswada wako kwa: kiswahiliprize@cornell.edu kabla ya muda uliowekwa kuisha. Tutaanza kupokea kazi kuanzia Aprili 5, 2022 hadi Juni 30, 2022.

Mwandishi mmoja anaweza kupeleka mswada mmoja tu katika kila kipengele.  Washindi hawaruhusiwi kushiriki kwa misimu miwili mfululizo tangu walipotangazwa kushinda.

  • Mswada wa riwaya usipungue maneno 50,000 na wa ushairi usipungue kurasa 60.
  • Kazi zote lazima ziwe za Kiswahili
  • Mswada unaweza kupelekwa kama faili ya Microsoft Word au Rich Text. Jina la mswada liwe jina la faili.
  • Ukurasa wa kwanza wa mswada uwe na  jina la mswada, na idadi ya maneno.
  • Mswada uchapishwe kwa mtindo wa Times New Roman, ukubwa wa pointi 12 na nafasi ya 1.5 kati ya mistari.
  • Mswada uambatishwe katika baruapepe.
  • Baruapepe iwe na maelezo yafuatayo: Jina rasmi,  jina la lakabu, nambari ya simu, tawasifu fupi, tarehe ya kuzaliwa, na nchi ya kuzaliwa na ya makazi/ utaifa na makazi.

 Kwa Wahariri: 

Tuzo ya Kiswahili ya Safal-Cornell ya Fasihi ya Kiafrika, yenye thamani ya jumla ya Dola za Marekani 15,000, hutolewa kila mwaka kwa miswada bora katika fani za riwaya, ushairi, mkusanyo wa hadithi fupi, riwaya za picha na wasifu. Miswada inayoshinda huchapishwa na mashirika ya uchapishaji vitabu, Mkuki na Nyota Publishers. Na mswada bora wa ushairi hufasiriwa kwa Kiingereza na kuchapishwa kitabu na shirika la Africa Poetry Book Fund.

Tuzo hii inadhaminiwa na kampuni ya Safal Mauritius Limited kupitia kampuni zake za Mabati Rolling Mills, Kenya, na kampuni ya ALAF Limited, Tanzania; pia na Ofisi ya Makamu wa Mkuu wa Maswala ya Kimataifa katika Chuo Kikuu cha Cornell, Idara ya Taaluma za Afrika ya Chuo Kikuu cha Cornell, Marekani, na Wakfu wa Ngugi wa Thiong’o (Ngugi wa Thiong’o Foundation).

Kampuni ya Safal Investments Mauritius Limited na matawi yake (ambayo ni pamoja na Mabati Rolling Mills Limited, Kenya, na ALAF Limited, Tanzania) inajulikana kwa jina la jumla la The Safal Group. Hii ni kampuni kubwa kabisa inayotengeneza mabati katika nchi 12 za Afrika. www.safalgroup.com

 

Mabati Rolling Mills Limited (MRM) ilibuniwa zaidi ya miaka 50 iliyopita. Ni kampuni kubwa kabisa Kenya inayotengeneza mabati ya kuezekea mapaa, na inaongoza katika utanzu huu wa ufundi. Pia inaongoza katika bara la Afrika kwa kutengeneza mabati ikitumia teknolojia ya hali ya juu kabisa inayopatikana duniani. Mabati yake maarufu yanasifika na yanaaminiwa na mamilioni ya wajenzi. www.mabati.com

 

Safal MRM Foundation, yenye makao yake Kenya, ni kitengo cha Mabati Rolling Mills na Safal Group kinachoshughulika na kutoa misaada ya aina mbalimbali. Miongoni mwa misaada hiyo, inayotolewa Mariakani, Kenya, ni kuanzisha na kuendelea kugharimia uendeshaji wa Taasisi ya Mabati ya Mafunzo ya Teknolojia (Mabati Technical Training Institute), na Kituo cha Mabati cha Matibabu (Mabati Medical Centre). www.safalmrmfoundation.org

 

ALAF Limited (ALAF) ni kampuni ya Tanzania inayoongoza katika utengenezaji wa mabati ya kuezekea mapaa. Tangu ilipobuniwa mwaka 1960, ALAF imeendelea kuchangia kwa kiasi kikubwa katika shughuli za ujenzi nchini. ALAF haitengenezi mabati ya kuezekea mapaa tu, bali pia aina za nyaya za chuma zinazotumika katika ujenzi wa mapaa. ALAF pia inatengeneza mabomba ya metali yanayotumika katika shughuli mbalimbali za ufundi. www.alaf.co.tz

 

Ofisi ya Makamu wa Mkuu wa Maswala ya Kimataifa katika Chuo Kikuu cha Cornell inatoa mwongozo na kusaidia kusimamia juhudi za kuzidisha shughuli za kimataifa Cornell. Lengo lake ni kushirikiana na shule, vyuo na taasisi nyengine ili kuendeleza na kutekeleza mipango inayohusiana na shughuli za kimataifa za Chuo Kikuu hiki. Ofisi hii inaisaidia Halmashauri mpya ya Kimataifa, ambayo mwenyekiti wake ni Makamu wa Mkuu. http://international.cornell.edu/international_vision

Idara ya Taaluma za Afrika na Utafiti inachangia kwa kiasi kikubwa katika shughuli za kitaaluma, kitamaduni na za kijamii kwenye Chuo Kikuu cha Cornell, Ithaca. http://www.asrc.cornell.edu

Ngugi Wa Thiong’o Foundation Wakfu huu unapata nguvu zake kutokana na hamu  na ari ya kukuza kuonekana kwa Lugha za Kiafrika nchini Kenya, barani Afrika, na duniani, na kutambuliwa kuwa ni vyombo mwafaka vya kuendeshea shughuli za sanaa ya uigizaji, ubunifu, uvumbuzi, na taaluma. Pia unazitambua lugha hizi kwamba zina uwezo wa kuwa mstari wa mbele katika kila fani – tangu utamaduni, sayansi za kibiolojia, teknolojia hadi tiba.   http://ngugiwathiongofoundation.org

Mkuki na Nyota Publishers ni shirika huru la uchapishaji vitabu vya kimaendeleo, kiukombozi, vya bei nafuu na maridadi. Shirika hili lilianzishwa mwaka 1991 kutokana na ukosefu wa vitabu vya kiwango cha juu nchini Tanzania. Kaulimbiu yake ni kuchapisha “Vitabu Vinavyofaa, Vitabu vya Bei Nafuu, na Vitabu Maridadi.” Disemba 2018 shirika hili liliichapisha diwani ya mshairi Dotto Rangimoto, Mwanangu Rudi Nyumbani, iliyoshinda nafasi ya kwanza ya ushairi katika mashindano haya ya mwaka 2017. Na mwezi wa Januari 2019 likaichapisha riwaya ya Ali Hilal Ali, Mmeza Fupa, iliyoshinda nafasi ya kwanza ya mashindano haya katika sehemu ya riwaya, mwaka 2017. http://www.mkukinanyota.com

Africa Poetry Book Fund inaimarisha na kuendeleza uchapishaji wa sanaa za kishairi kupitia vitabu vyake, mashindano, warsha, semina, pamoja na kushirikiana na wachapishaji, matamasha, mawakala, vyuo, vyuo vikuu, makongamano, na vikundi vingine vinavyohusika na ushairi Afrika. http://africanpoetrybf.unl.edu/

Bodi ya Wadhamini: Abdilatif Abdalla (Mwenyekiti), Mukoma Wa Ngugi, Lizzy Attree, Walter Bgoya, Sarit Shah, Henry Chakava, Chege Githiora, Clarissa Vierke, Farouk Topan, Carole Boyce Davies, and Ngugi Wa Thiong’o.

Msimamizi (Director): Moses Kilolo

Mawasiliano:

Prof. Mukoma Wa Ngugi, Cornell University, kiswahiliprize@cornell.edu

Moses Kilolo  kiswahiliprize@cornell.edu

Logos for Sponsors & Partners

Skip to toolbar