Tangazo la Washindi wa 2023

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI:

WITO WA KUWASILISHA MISWADA KATIKA TUZO YA KISWAHILI YA SAFAL-CORNELL YA FASIHI YA AFRIKA –  KWA MWAKA 2023

Nairobi, Kenya, 27 Machi 2023… Tuzo ya Kiswahili ya Safal-Cornell ya Fasihi ya Afrika leo imetangaza wito wa kuwasilisha miswada kwa ajili ya shindano la nane la Tuzo hii, ambayo hapo awali iliitwa Tuzo ya Kiswahili ya Mabati-Cornell ya Fasihi ya Afrika. Kuanzia mwaka jana, jina lake lilibadilishwa ili kuakisi jina la kampuni-mama, ambayo ndiyo mdhamini mkuu – yaani kampuni ya Safal Group (Mauritius) Limited, kupitia kampuni zake tanzu za Mabati Rolling Mills (MRM) ya Kenya, na ALAF Limited ya Tanzania. Safal Group ni kampuni kubwa inayotengeneza vifaa vya  ujenzi barani Afrika, na ina matawi  katika nchi 8.

Tuzo ya Kiswahili ya Safal-Cornell ya Fasihi ya Afrika ilianzishwa mwaka 2014 na Dkt. Lizzy Attree na Dkt. Mukoma wa Ngugi ili kutambua uandishi kwa lugha za Kiafrika na pia kuhimiza tafsiri baina ya lugha za Kiafrika zenyewe kwa zenyewe, na pia kutafsiri maandishi ya lugha nyengine kwa lugha za Kiafrika. Katika kipindi cha miaka yote hii, Tuzo ya Kiswahili ya Safal-Cornell ya Fasihi ya Afrika pia imewasaidia waandishi walioshiriki katika mashindano ya Tuzo hii kwa maandishi yao kuchapishwa vitabu.

Wakati juhudi za kuhimiza kusoma na kuandika kwa Kiswahili zinaendelea, tunawahimiza waandishi kutoka Afrika Mashariki na nchi nyengine za Afrika kuwasilisha miswada yao na kushiriki katika shindano la mwaka huu.

Tuzo ya Kiswahili ya Safal-Cornell ya Fasihi ya Afrika inauthamini uungwaji mkono mkubwa wa Safal Group katika kusaidia kuiendeleza Fasihi ya Afrika. Katika mwezi wa Januari mwaka huu, washindi wa Tuzo hii wa shindano la mwaka 2022 walitangazwa katika sherehe maalumu iliyofanyika jijini Dar es Salaam ambapo mgeni rasmi alikuwa ni Mheshimiwa Majaliwa Kassim Majaliwa, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Wanaotaka kushiriki katika shindano la mwaka huu wanahimizwa kuiwasilisha miswada yao ambayo haijachapishwa, katika tanzu za riwaya, ushairi, mkusanyo wa hadithi fupi, wasifu  na riwaya za picha. Vitabu vilivyokwisha chapishwa havitazingatiwa. Zawadi za jumla ya Dola 15,000 za Marekani zitatolewa kama ifuatavyo: mshindi wa kwanza katika utanzu wa riwaya na ushairi kila mmojawao atapata Dola 5,000; na washindi wa nafasi ya pili katika utanzu wa riwaya au ushairi, au utanzu wowote mwengine, watapata zawadi ya Dola 2,500 kila mmoja.

Miswada itakayoshinda itachapishwa vitabu na shirika la uchapishaji la Mkuki na Nyota Publishers (Tanzania), ambalo linaweza kushirikiana na wachapishaji wengine ili kurahisisha upatikanaji wa vitabu vilivyoshinda. Vitabu vya miswada ya ushairi itakayoshinda vitafasiriwa kwa Kiingereza na kuchapishwa na Africa Poetry Book Fund.

Sherehe ya kuwapa zawadi washindi wa mwaka 2023 itafanyika Januari 2024, na waandishi wote walioorodheshwa watahudhuria.

Mwongozo wa Uwasilishaji:

Wanaotaka kushiriki wanaombwa wapeleke miswada yao kwa anwani hii: kiswahiliprize@cornell.edu. Tarehe ya mwisho ya kupokewa miswada ni 30 Juni, 2023. Kwa maelezo zaidi – kwa Kiswahili na Kiingereza – tafadhali tembelea  tovuti yetu https://kiswahiliprize.cornell.edu.

 

Bodi ya Wadhamini: Abdilatif Abdalla (Mwenyekiti), Mukoma Wa Ngugi, Lizzy Attree, Walter Bgoya, Sarit Shah, Anthony Ng’ang’a, Henry Chakava, Chege Githiora, Clarissa Vierke, Farouk Topan, Carole Boyce Davies, and Ngugi Wa Thiong’o.

Mkurugenzi: Munyao Kilolo

Tovuti: http://blogs.cornell.edu/kiswahiliprize/

Twitter: @KiswahiliPrize

Facebook: https://www.facebook.com/pages/Mabati-Cornell-Kiswahili-Prize for

African-Literature/1534905843433822

Mawasiliano: Prof. Mukoma Wa Ngugi, Cornell University, kiswahiliprize@cornell.edu Dr. Lizzy Attree, kiswahiliprize@cornell.edu, Moses Kilolo  kiswahiliprize@cornell.edu.

 

 

 

Skip to toolbar