Washindi wa mwaka 2021 ni

TUZO YA KISWAHILI YA MABATI-CORNELL

YA FASIHI YA AFRIKA

 Tangazo la Washindi wa 2021

 

Washindi wa Tuzo ya Kiswahili ya Mabati-Cornell ya Fasihi ya Afrika kwa mwaka 2021 walitangazwa tarehe 27 Januari, 2021, kwenye hafla maalumu iliyofanyika katika Ukumbi wa Mlimani City, Dar es Salaam, ambapo Mgeni Rasmi alikuwa Mheshimiwa Kassim Majaliwa, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Washindi hao walitangazwa na Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini ya Tuzo ya Kiswahili ya Mabati-Cornell ya Fasihi ya Afrika Abdilatif Abdalla. Miongoni mwa wageni mashuhuri waliokuwepo ni pamoja na Mheshimiwa Mohammed Omar Mchengerwa, Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo; Mheshimiwa Amos Makalla, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, na Bwana Anders Lindgren, Mkurugenzi Mtendaji wa Safal Group.

Madhumuni makuu ya Tuzo hii, iliyoanzishwa mwaka 2014 na Dkt. Lizzy Attree (Short Story Day Africa) na Dkt. Mukoma wa Ngugi (Chuo Kikuu cha Cornell, Marekani), ni kuthamini uandishi kwa lugha za Kiafrika, kuhimiza sanaa ya tafsiri baina ya lugha za Kiafrika zenyewe kwa zenyewe, na pia kutafsiri maandishi ya lugha nyengine kwa lugha za Kiafrika.

Washindi:

Katika Kitengo cha Riwaya, mshindi wa nafasi ya kwanza ni  Halfani Sudy kwa riwaya yake inayoitwa Kirusi Kipya. Na mshindi wa kwanza katika Kitengo cha Ushairi ni Mohamed Omar Juma kwa diwani yake inayoitwa Chemchemi Jangwani.  Mshindi wa nafasi ya pili

katika Kitengo cha Riwaya ni Lucas Lubago kwa riwaya yake, Bweni la Wasichana. Kama ilivyotangazwa wakati Tuzo hii ilipoanzishwa, mshindi wa nafasi ya pili anaweza pia kutoka katika kitengo chochote. Kwa sababu hiyo, majaji walimchagua Mbwana Kidato kushika nafasi hiyo kwa mswada wake uitwao Sinauba, ambao majaji waliyaeleza maandishi hayo kuwa ni ya mtindo mpya. Kwa niaba yao, Prof Mutembei alisema, “Kazi hii ni aina mpya ya uandishi. Ni uandishi wa kiubunifu wa hali ya juu; lakini si riwaya, si tamthilia. Yote mawili yamo: mna uandishi wa kinathari (kama riwaya) na mna majibizano na maongezi baina ya wahusika (kama tamthilia). Ni kwa sababu hiyo kazi hii tuliipa nafasi maalumu ya thamani.

Mshindi wa nafasi ya kwanza katika kila kitengo alitunukiwa Dola 5,000 za Marekani; na mshindi wa pili katika kila kitengo alipokea Dola 2,500 za Marekani.

Majaji wa mashindano ya mwaka 2020 walikuwa ni  Prof. Aldin K. Mutembei (Chuo Kikuu cga Dar es Salaam), Dkt. Salma Omar Hamad (Chuo Kikuu Huria cha Tanzania) na Dkt. Joseph N. Maitaria (Chuo Kikuu cha Karatina, Kenya). Mwenyekiti wa Jopo la Majaji, Prof. Aldin K. Mutembei, alisema kwa niaba ya wenzake, “Miswada iliyoshinda ilikuwa ni ya kiwango cha juu cha ubunifu, matumizi sahihi na ubora wa lugha, na ushirikishwaji wa wahusika wenye uhalisia katika jamii. Pia tulizingatia maudhui yanayolingana na majira ya nyakati hizi tulizonazo katika jamii zetu Afrika.Mfupi”

Wasifu Mfupi wa Washindi:

Halfani Sudy alizaliwa mwaka 1989, mkoani Lindi, wilaya ya Kilwa. Amekuwa akiandika riwaya tangu mwaka 2014, na ameshachapisha vitabu vitano: Penzi Chungu, Farida, Kipepeo Mwekundu, Kanda ya Siri na Msako Hatari. Hivi sasa, Halfani Sudy ni Mkuu wa Idara ya Ustawi wa Jamii, na anasomesha somo la Ustawi wa Jamii katika chuo cha New Mafinga Health Allied Institute kilichopo Mafinga, mkoani Iringa.

Mohamed Omar Juma alizaliwa mwaka 1986 katika kijiji cha Wambaa, mkoa wa kusini Pemba. Ana shahada ya kwanza ya Sanaa na Ualimu (B.A. Ed) kutoka Chuo Kikuu cha Waislamu, Morogoro, Tanzania, alikosomea somo la Kiswahili na Kiingereza. Mwaka 2018 alitunukiwa cheti katika mashindano ya Tuzo ya Ushairi ya Ebrahim Hussein. Hivi sasa ni mwalimu wa Kiswahili na Kiingereza katika Shule ya Sekondari ya Minazini, Kigamboni,  Dar es Salaam; na pia ni Mwanafunzi wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania, anakosomea Shahada ya Uzamili: Elimu katika Utawala, Mipango na Mafunzo ya Sera.

Kama ilivyotangazwa mwezi wa Disemba 2020, wafuatao ni miongoni mwa waliokuwemo katika Orodha Fupi: Hafidh Athumani Kido kwa riwaya yake, Kanzu ya UkubwaMsusa Mohamedi Msusa kwa diwani yake, Malenga wa Masasi; na Mfaume Hamisi Mfaume kwa diwani yake, Sinaye Baba.

Kwa Wahariri: 

Tuzo ya Kiswahili ya Mabati-Cornell ya Fasihi ya Afrika, yenye thamani ya jumla ya Dola za Marekani 15,000, hutolewa kila mwaka kwa miswada bora, au kwa vitabu vilivyochapishwa miaka miwili kabla ya mwaka wa kutolewa zawadi, katika fani za riwaya, ushairi, wasifu, tamthilia na riwaya za picha. Miswada inayoshinda huchapishwa na mashirika ya uchapishaji vitabu, Mkuki na Nyota Publishers, Tanzania, na East African Educational Publishers (EAEP), Kenya. Na mswada bora wa ushairi hufasiriwa kwa Kiingereza na kuchapishwa kitabu na shirika la Africa Poetry Book Fund.

Tuzo hii inadhaminiwa na kampuni ya Mabati Rolling Mills, Kenya, na kampuni ya ALAF Limited, Tanzania (ambazo ni miongoni mwa kampuni za Safal Mauritius Limited); pia na Ofisi ya Makamu wa Mkuu wa Maswala ya Kimataifa katika Chuo Kikuu cha Cornell, Idara ya Taaluma za Afrika ya Chuo Kikuu cha Cornell, Marekani, na Wakfu wa Ngugi wa Thiong’o (Ngugi wa Thiong’o Foundation).

Kampuni ya Safal Investments Mauritius Limited na matawi yake (ambayo ni pamoja na Mabati Rolling Mills Limited, Kenya, na ALAF Limited, Tanzania) inajulikana kwa jina la jumla la The Safal Group. Hii ni kampuni kubwa kabisa inayotengeneza mabati katika nchi 12 za Afrika. www.safalgroup.com

Mabati Rolling Mills Limited (MRM) ilibuniwa zaidi ya miaka 50 iliyopita. Ni kampuni kubwa kabisa Kenya inayotengeneza mabati ya kuezekea mapaa, na inaongoza katika utanzu huu wa ufundi. Pia inaongoza katika bara la Afrika kwa kutengeneza mabati ikitumia teknolojia ya hali ya juu kabisa inayopatikana duniani. Mabati yake maarufu yanasifika na yanaaminiwa na mamilioni ya wajenzi. www.mabati.com

Safal MRM Foundation, yenye makao yake Kenya, ni kitengo cha Mabati Rolling Mills na Safal Group kinachoshughulika na kutoa misaada ya aina mbalimbali. Miongoni mwa misaada hiyo, inayotolewa Mariakani, Kenya, ni kuanzisha na kuendelea kugharimia uendeshaji wa Taasisi ya Mabati ya Mafunzo ya Teknolojia (Mabati Technical Training Institute), na Kituo cha Mabati cha Matibabu (Mabati Medical Centre). www.safalmrmfoundation.org

ALAF Limited (ALAF) ni kampuni ya Tanzania inayoongoza katika utengenezaji wa mabati ya kuezekea mapaa. Tangu ilipobuniwa mwaka 1960, ALAF imeendelea kuchangia kwa kiasi kikubwa katika shughuli za ujenzi nchini. ALAF haitengenezi mabati ya kuezekea mapaa tu, bali pia aina za nyaya za chuma zinazotumika katika ujenzi wa mapaa. ALAF pia inatengeneza mabomba ya metali yanayotumika katika shughuli mbalimbali za ufundi. www.alaf.co.tz

Ofisi ya Makamu wa Mkuu wa Maswala ya Kimataifa katika Chuo Kikuu cha Cornell inatoa mwongozo na kusaidia katika kusimamia juhudi za kuzidisha shughuli za kimataifa Cornell. Lengo lake ni kushirikiana na shule, vyuo na taasisi nyengine ili kuendeleza na kutekeleza mipango inayohusiana na shughuli za kimataifa za Chuo Kikuu hiki. Ofisi hii inaisaidia Halmashauri mpya ya Kimataifa, ambayo mwenyekiti wake ni Makamu wa Mkuu. http://international.cornell.edu/international_vision

Idara ya Taaluma za Afrika na Utafiti inachangia kwa kiasi kikubwa katika shughuli za kitaaluma, kitamaduni na za kijamii kwenye Chuo Kikuu cha Cornell, Ithaca. http://www.asrc.cornell.edu

Ngugi Wa Thiong’o Foundation Wakfu huu unapata nguvu zake kutokana na hamu na ari ya kukuza kuonekana kwa Lugha za Kiafrika nchini Kenya, barani Afrika, na duniani, na kutambuliwa kuwa ni vyombo mwafaka vya kuendeshea shughuli za sanaa ya uigizaji, ubunifu, uvumbuzi, na taaluma. Pia unazitambua lugha hizi kwamba zina uwezo wa kuwa mstari wa mbele katika kila fani – tangu utamaduni, sayansi za kibiolojia, teknolojia hadi tiba.   http://ngugiwathiongofoundation.org

East African Educational Publisher (EAEP) ni shirika mojawapo kuu la wachapishaji. EAEP linajitahidi kuyahusisha maadili yanayoonekana kama kwamba yanakinzana; yaani kuchapisha kazi za kiwango cha juu zinazogusia maswala ya kijamii, ya kitamaduni na ya kiuchumi, na wakati huo huo kufaulu kufanya biashara iliyo tayari kukabiliana na hali halisi na misukosuko ya zama za kiteknolojia. http://www.eastafricanpublishers.com

Mkuki na Nyota Publishers ni shirika huru la uchapishaji vitabu vya kimaendeleo, kiukombozi, vya bei nafuu na maridadi. Shirika hili lilianzishwa mwaka 1991 kutokana na ukosefu wa vitabu vya kiwango cha juu nchini Tanzania. Kaulimbiu yake ni kuchapisha “Vitabu Vinavyofaa, Vitabu vya Bei Nafuu, na Vitabu Maridadi.” Disemba 2018 shirika hili liliichapisha diwani ya mshairi Dotto Rangimoto, Mwanangu Rudi Nyumbani, iliyoshinda nafasi ya kwanza ya ushairi katika mashindano haya ya mwaka 2017. Na mwezi wa Januari 2019 likaichapisha riwaya ya Ali Hilal Ali, Mmeza Fupa, iliyoshinda nafasi ya kwanza ya mashindano haya katika sehemu ya riwaya, mwaka 2017. http://www.mkukinanyota.com

Africa Poetry Book Fund inaimarisha na kuendeleza uchapishaji wa sanaa za kishairi kupitia vitabu vyake, mashindano, warsha, semina, pamoja na kushirikiana na wachapishaji, matamasha, mawakala, vyuo, vyuo vikuu, makongamano, na vikundi vingine vinavyohusika na ushairi Afrika. http://africanpoetrybf.unl.edu/

Bodi ya Wadhamini: Abdilatif Abdalla (Chair), Mukoma Wa Ngugi, Lizzy Attree, Walter Bgoya, Henry Chakava, Chege Githiora, Clarissa Vierke, Farouk Topan, Carole Boyce Davies, and Ngugi Wa Thiong’o.

Msimamizi (Administrator): Moses Kilolo

Majaji wa 2020

Prof. Aldin K. Mutembei (Shahada ya Kwanza (Elimu).; Shahada ya Uzamili (Isimu) (Dar); Shahada ya Uzamili (Fasihi); Shahada ya Uzamivu (Leiden) ni Mgoda, Kigoda cha Uprofesa wa Kiswahili cha Mwalimu Julius Nyerere, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. Kabla ya hapo alikuwa Mkurugenzi wa Taasisi ya Taaluma za Kiswahili; na sasa ni Mkurugenzi wa Taasisi ya Confucius, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. Anasomesha Fasihi ya Kiswahili/Kiafrika, Mawasiliano, Nadharia za Uhakiki, Fasihi Simulizi na Lugha ya Kiswahili kwa wazungumzaji wa lugha nyengine. Ameshachapisha vitabu vine, miongoni mwa hivyo ni riwaya Kisiki Kikavu (E & D Limited, 2005) na Korasi Katika Fasihi: Nadharia Mpya ya Uhakiki (Taasisi ya Taaluma za Kiswahili, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, 2012).

Dkt. Salma Omar Hamad alizaliwa Pemba, Zanzibar, mwaka 1980. Hivi sasa ni Mhadhiri wa Fasihi ya Kiswahili na Isimu katika Chuo Kikuu Huria cha Tanzania. Alipata shahada yake ya kwanza ya Kiswahili (Elimu) kutoka Chuo Kikuu cha Taifa Zanzibar (SUZA); na Shahada ya Uzamili (Isimu) kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Shahada yake ya Uzamivu  katika Kiswahili aliipata kutoka Chuo Kikuu cha Taifa Zanzibar. Dkt. Salma ameandika hadithi fupi kadhaa zilizoko kwa wachapishaji zikisubiri kuchapishwa. Pia amechangia hadithi katika mikusanyo ya hadithi fupi; kama vile hadithi yake, “Shibe Inatumaliza” kwenye mkusanyo uitwao Tumbo Lisiloshiba na Hadithi Nyingine (Longhorn Publishers, 2016).

Dkt. Joseph N. Maitaria ni Mhadhiri Mwandamizi na Mkuu wa Idara ya Sanaa na Lugha, Kitivo cha Elimu na Sayansi za Kijamii, Chuo Kikuu cha Karatina, Kenya. Ana shahada ya Kwanza ya Ualimu (Chuo Kikuu cha Kenyatta) ambapo alisomea Shahada ya Elimu, Kiswahili na Dini. Shahada ya Uzamili alisomea Fasihi ya Kiswahili (Chuo Kikuu cha Kenyatta), na Shahada ya Uzamivu kuhusu Ushairi wa Kiswahili (Chuo Kikuu cha Kenyatta). Yeye pia ni mwanachama na Katibu wa vyama vya kitaaluma vya Kiswahili, kama vile Chama cha Kiswahili cha Afrika Mashariki (CHAKAMA) na Chama cha Kiswahili cha Taifa (CHAKITA), Kenya. Dkt. Maitaria amechapisha vitabu na makala kadhaa kuhusu Fasihi ya  Kiswahili kwenye majarida ya kitaaluma.

Mawasiliano:

Prof. Mukoma Wa Ngugi, Cornell University, kiswahiliprize@cornell.edu

Dr Lizzy Attree, kiswahiliprize@cornell.edu

Moses Kilolo  kiswahiliprize@cornell.edu

Skip to toolbar