Tuzo Maalumu kwa mwaka 2021

Tuzo ya Nyabola ya Sayansi Bunilizi na Kidhana za Kiswahili, Mwaka 2021. Tangazo la Orodha Fupi

Orodha fupi ya Tuzo ya Nyabola ya Sayansi Bunilizi na Kidhana, ikishirikiana na Tuzo ya Mabati Cornell ya Fasihi ya Afrika imetangazwa rasmi na kamati ya Majaji leo Jumatano, Tarehe 17, Novemba 2021.

Tuzo ya waandishi vijana iliyoiasisiwa na Bi Nanjala Nyabola mwaka 2021, ina lengo maalum la kuwatambua waandishi kazi za Hadithi Fupi za Kiswahili za Sayansi Bunilizi na Kidhana kwa madhumuni ya kuendeleza msamiati wa sayansi na teknolojia kwa Kiswahili. Waandishi walihimizwa kutumia sayansi bunilizi na Kidhana kuonyesha matumizi ya msamiati wa sayansi na teknolojia kwa Kiswahili. “Tulitiwa motisha sana na kazi nyingi za hadithi za Sayansi Bunilizi tulizopokea zenye visa na maudhui anuwai. Ilikuwa tajriba nzuri na ya mara ya kwanza. Tunatarajia kuwa tuzo hii itaendelea kukua zaidi.” Alisema Bi Nyabola.

Waadishi ambao wamefanikiwa kuorodheshwa katika orodha Fupi ni wafuatao: (majina yamepangwa kialfabeti kulingana na jina la mwisho):

• Sofi Binsari (Kenya) Dunia ya Pili
• Twihuvila Gillah (Kenya) Pigo Zito
• Hussna Mohamed Hassan (Tanzania) Afriti Hasitiki
• Stallone Joyfully (Tanzania) Dubwasha
• Emmanuel Kimeu (Kenya) Sayari Ya Wanawake
• Hassan Omar Mambosasa (Tanzania) Mashine
• Haruni Manigu (Tanzania) Ustaarabu Wa Sayari Ya Sadiza
• Charles John Mlowezi (Tanzania) Kamera Ya Mtoisa
• Shabani Omari Molito (Tanzania) Mgeni Kutoka Sayari Nyekundu
• Florence Chanya Mwaita (Kenya) Miongo Mia Moja

Tungo 147 zilizotumwa kwa tuzo hii zilisomwa na majaji kama vile Dkt. Hamisi Babusa ambaye ni mhadhiri wa Lugha ya Kiswahili katika Chuo Kikuu cha Kenyatta, Nairobi, Kenya. “Baadhi ya Hadithi ziliandikwa na waandishi ambao asili ya nchi zao si za wazungumzaji wa Kiswahili. Hili linaonyesha kuwa lugha ya Kiswahili inaendelea kuwa maarufu zaidi ulimwenguni.” Alisema Dkt. Babusa. Washindi wa Tuzo ya Nyabola watatangazwa mwakani, Tarehe 28, Januari, 2022. Mkusanyiko wa Hadithi ishirini bora utachapishwa na kutolewa mwishoni mwa mwaka 2022.

Vidokezo kwa Wahariri
Tuzo hii inadhaminiwa kimsingi na Bi Nyabola kupitia Jamii ya Kidijitali ya Stanford na inatekelezwa kwa kushirikiana na Tuzo ya Fasihi ya Mabati Cornell ya Lugha za Kiafrika.

Majaji 2021
Dr. Hamisi Babusa ni mhadhiri wa Kiswahili na Ufundishaji Lugha. Amefunza katika vyuo vikuu vingi vikiwemo Chuo Kikuu cha St. Lawrence, kilicho CANTON, NY, Marekani. Kwa sasa ni mhadhiri na Mkuu wa Kitengo katika Chuo Kikuu cha Kenyatta. Mbali na kuwa mhadhiri, Dkt. Babusa pia ni mwandishi kazi za kibunilizi na za Kitaaluma. Ameandika kazi anuwai kama vile Kamusi Teule na pia A Dictionary of English and Swahili Equivaleny Proverbs na nyingine nyingi. Amechangia katika mikusanyiko mingi ya Hadithi Fupi na Mashairi na pia akahariri kadhaa. Dkt. Babusa pia ameandika novela za watoto kama vile MSURURU WA BINTI KITABU na MSURURU WA MAKUMBA. Yeye ndiye mwandishi wa kwanza kuwahi kutunga hadithi za Kiswahili za Sayansi Bunilizi MSURURU WA MAKUMBA ambazo zilimfanya akapewa tuzo ya kuwa mmoja wa wanasayansi ishirini bora nchini Kenya, Mwaka 2018. Aidha yeye ndiye mwasisi na Meneja Msimamizi wa BABUSA TV, chaneli ya mtandaoni ya kufunza watoto lugha ya Kiswahili kwa kupitia vikaragosi na nyimbo.

Bi Nanjala Nyabola ni mwandishi na pia mchambuzi wa masuala ya kisiasa, nchini Kenya. Ametunga “Digital Demcoracy, Analogue Politics: How the Internet Era is Transforming Politics in Kenya” (kilichochapishwa na Zed Books, mwaka 2018) na “Travelling While Black: Essays Inspired by a Life on the Move” (kilichochapishwa na Hurst, mwaka 2020).


TUZO YA KISWAHILI YA MABATI-CORNELL

YA FASIHI YA AFRIKA na

TUZO YA NYABOLA YA UANDISHI WA HADITHI 

ZA KISAYANSI NA ZA KIDHANA KWA KISWAHILI 2021

Tuzo ya Kiswahili ya Mabati-Cornell ya Fasihi ya Afrika inatangaza Tuzo Maalumu kwa mwaka 2021 kwa vijana wenye umri wa baina ya  miaka  18 na 35 kuandika hadithi za kisayansi na za kidhana. Kwa kushirikiana na mwandishi na mchambuzi wa kisiasa, Nanjala Nyabola, lengo la Tuzo hii ni kuendeleza na kueneza matumizi ya msamiati wa kiteknolojia na kidijitali katika jamii zinazotumia lugha ya Kiswahili.

Hadithi zenye urefu wa baina ya maneno 2,000 na 2,500 ziandikwe kwa Kiswahili Sanifu, na zisiwe ni tafsiri kutoka lugha nyengine. Hadithi kumi bora zitakusanywa na kuchapishwa katika kitabu. Washindi watatunukiwa zawadi zifuatazo:

Mshindi wa Kwanza – Dola za Marekani $1,000

Mshindi wa Pili – Dola za Marekani $500

Mshindi wa Tatu – Dola za Marekani $250

Hadithi zitakazopelekwa kwenye mashindano haya ziandikwe kuwa ni kwa ajili ya Tuzo ya Nyabola ya Uandishi wa Hadithi za Kisayansi na za Kidhana; na zipelekwe kwenye anwani: kiswahiliprize@cornell.edu kabla ya tarehe 31 Mei, 2021.

“Tuzo za Fasihi husaidia kuibua vipawa vipya, na kuwahamasisha wengine kuanza kuandika; na wakati huo huo kuwadhihirishia wasomaji uzuri, utajiri na ufinyangaji wa lugha za waandishi hao na pia kuwapa waandishi nyenzo za kuzitumia katika kujieleza na kushiriki katika mawanda mapya,” anasema Munyao Kilolo wa Tuzo ya Kiswahili ya Mabati-Cornell.

Nyabola Nanjala anaongeza kwa kusema, “Hadithi za kubuni za kisayansi na za kidhana huwapa vijana ujasiri wa kuzibomoa kuta zinazowawekea vikwazo vya kutokuwa na mawazo ya kufikiria mustakbali wao kwa namna iliyo bora. Maandishi ya kubuni ya kisayansi na ya kidhana yamesaidia katika uvumbuzi wa akili-dijitali (artificial intelligence), maadili ya kiteknolojia na maadili ya kisiasa, pamoja na kuchochea kuihakiki mienendo ya kisiasa, kwa mfano katika kitabu cha Isaac Asimov, Three Rules of Robotics (Kanuni Tatu za Kiroboti); na pia jinsi ya kuudadisi uwezo na madaraka ya dola, kama alivyofanya George Orwell katika kitabu chake kiitwacho 1984. Kwa hakika, baadhi ya maendeleo makubwa yaliyotokea katika nyakati zetu hizi yalitokana na ilhamu za hadithi za kisayansi na kidhana.”

Kiswahili kinazungumzwa na zaidi ya watu milioni 140 kuanzia Mashariki ya  Afrika mpaka Kusini mwa Afrika, na ndiyo lugha ya Afrika iliyoenea zaidi duniani. Ingawa Kiswahili kina historia ndefu ya kazi za kitamaduni na za uandishi, kama vile ushairi na tungo nyenginezo, lakini kimechelewa kutumiwa kwa wingi katika kutafsiria na  kuenezea lugha ya kiteknolojia – kama zilivyo lugha nyengine zisizokuwa Kiingereza. Bila ya kuwa na lugha kama hiyo ya kiteknolojia, nchi za Afrika zitaendelea kutengwa kando badala ya kuwa katika kiwango kimoja na nchi nyengine duniani. Kwa kuwa Kiswahili ni lugha iliyokita mizizi duniani na ambayo ina uwezo wa kutumiwa kwa matumizi mapana, ni muhimu kuongeza juhudi za kuifanya lugha hii na wazungumzaji wake kuwa bega kwa bega na maenedeleo ya haraka yanayotokea katika uwanja wa teknolojia.

Kwa hivyo, lengo la Tuzo hii ni kuwahimiza na kuwapa moyo waandishi wabunifu wa Kiswahili wa kizazi cha sasa na kijacho, na wakati huo huo kuendeleza na kuikuza lugha ya kiteknolojia na haki za kidijitali.

Warsha

Ili kuwasaidia na kuwapa miongozo wale wanaotaka kushiriki katika mashindano haya, katika miezi ya Machi, Aprili na Mei, 2021, waandalizi wa Tuzo hii watafanya warsha tatu kuhusu uandishi wa hadithi za kidhana. Si lazima kushiriki katika warsha hizi zitakazofanywa mtandaoni, lakini washiriki wanaweza kufaidika kwa kupata mbinu na uthubutu utakaowasaidia wale wanaotaka kushiriki katika mashindano haya.

Tafadhali wasiliana nasi kupitia kiswahiliprize@cornell.edu iwapo utataka maelezo zaidi.

Skip to toolbar