Mukoma Wa Ngugi, mwanzilishi mmoja, ni Profesa wa Kiingereza katika Chuo Kikuu cha Cornell na mwandishi wa Black Star Nairobi (Melville, 2013) na Nairobi Heat (Penguin, SA 2009, Melville House Publishing, 2011) na diwani ya mashari iitwayo Hurling Words at Consciousness (AWP, 2006). Yeye ni mwandishi wa This is Africa. Mukoma ana Shahada ya Udaktari katika Kiingereza kutoka Chuo Kikuu cha Wisconsin, Madison, Shahada ya Ufundi (MA) katika Uandishi wa Kubuni kutoka Chuo Kikuu cha Boston na Digrii ya Kiingereza na Sayansi ya Siasa kutoka Chuo cha Albright. Jarida la New African lilimtaja kama mmojawapo wa Waafrika 100 wenye wadhifa 2013.
Tafsiri ya Kijerumani ya Nairobi Heat ilitambuliwa na Buchkultur kama Kitabu cha Riwaya ya Uhalifu cha Msimu. Mwaka wa 2009, aliteuliwa mmojawapo wa washindi waliopendekezwa kushinda Caine Prize for African Writing Tuzo ya Caine ya Uandishi wa Kiafrika na mwaka wa 2010 kwa Penguin Prize for African Writing kwa nakala ya riwaya yake, The First and Second Books of Transition. Riwaya mpya inayoitwa Mrs. Shaw itachapishwa karibuni na Ohio U/Swallow Press na Hunting Words with my Father (mashairi) kutoka Akiba ya Afrika ya Ushairi mwaka wa 2016. Tafsiri ya Kijerumani ya Black Star Nairobi itachapishwa karibuni.
Lizzy Attree, mmojawapo wa waanzilishi wa Tuzo hii, ana shahada ya uzamivu (PhD) kutoka School of Oriental and African Studies (SOAS), Chuo Kikuu cha London, kuhusu “Majibu ya Fasihi kwa Virusi vya Ukimwi Kutoka Afrika Kusini na Zimbabwe, 1990 – 2005”. Mkusanyo wake wa mahojiano na waandishi wa kwanza wa Kiafrika walioandika kuhusu Virusi na Ukimwi kutoka Zimbabwe na Afrika Kusini, uitwao Blood on the Page (Damu Ukurasani), ulichapishwa na Cambridge Scholars Publishing mwaka 2010. Mnamo mwaka huo huo alikuwa Mhadhiri kwenye Idara ya Kiingereza, Chuo Kikuu cha Rhodes, Afrika Kusini. Mwaka 2015 alisomesha Fasihi ya Afrika katika Chuo cha Kings College, London. Hivi sasa anasomesha Fasihi ya Ulimwengu na Fasihi ya London ya Kisasa, huko Richmond, Chuo Kikuu cha Kimataifa cha Marekani, London. Yeye ni Mkurugenzi kwenye bodi ya Short Story Day Africa; na kuanzia mwaka 2014 mpaka 2018 alikuwa Mkurugenzi wa Tuzo ya Caine. Pia amewahi kuwa mwamuzi wa Folktales Re-Imaged mtandaoni. Lizzy Attree pia ni mtayarishaji wa ‘Kufikiria Nje ya Eneo la Penalti’ (mradi wa Wachezaji Mpira wa Kiafrika unaofadhiliwa na Baraza la Sanaa la Uingereza na kuungwa mkono na Jumuiya ya Ushairi); na ni mwandishi na mhakiki.
Abdilatif Abdalla anajulikana zaidi kwa diwani yake ya mashairi ‘Sauti ya Dhiki’ (iliyochapishwa mwaka wa 1973) iliyoandikwa akiwa gerezani Kenya katika ya miaka 1969 na 1972. Alitiwa jela kwa kuandika kijitabu muhimu ‘Kenya: Twendapi?’ (1968) iliyoshutumu ukandamizaji wa serikali ya KANU ya Jomo Kenyatta. Abdalla pia amehusika na miradi mengi ya utafsiri na uhariri wa riwaya za baada ya ukoloni (Ayi Kwei Armah), tafsiri za Kurani, mashairi ya Kiswahili cha kale na kazi muhimu za kitaalimu huku akisimamia upinzani dhidi ya uongozi wa Moi alipokuwa uhamishoni London (na kina Ngugi) miongo ya 1980 na 1990.
Walter Bgoya, mwaka wa 1972 hadi 1990, Walter Bgoya alisimamia Nyumba ya Uchapishaji Tanzania (Tanzania Publishing House, TPH) iliyoimarisha Dar es Saleem kama eneo liloendelea kwa wasomi kimataifa. Mifano ya chapisho za TPH ni “How Europe Underdeveloped Africa” (Jinsi Ulaya Iliimaskinisha Afrika) ya Walter Rodney, “Sacred Hope” (Tumaini Tukufu) ya Agostinho Neto, “Establishing People’s Power to Serve the Masses” (Kuanzisha Nguvu za Umma Kuihudumia Jamii) ya Samora Machel na “Class Struggle in Tanzania” ( Vita vya Kitabaka Tanzania) ya Issa Shivji. Mwaka wa 1991, Bgoya alianzisha Mkuki na Nyota, kampuni huru ya kuchapisha vitabu ilioko Dar es Salaam. Bgoya alisema, kama jawabu kwa kutokuwa na uchapishaji huru wa kitaalimu Tanzania: “Tunajivunia kuchapisha vitabu muhimu, maridadi na vya bei rahisi na kuviweka kwenye mikono ya wasomi wenye hamu Tanzania na duniani.” Vitabu vya Mkuki na Nyota, vitabu vya watoto, vitabu vya biashara ya umma na vitabu vya elimu kwa Kiingereza na Kiswahili. Mchapishaji huyu anajitahidi kutafsiri fasihi kwa Kiswahili kwa mfano kitabu Kibwana Mdogo (The Little Prince) iliyo na asili ya Kifaransa. Bgoya ni mmoja wa waanzilishi wa Kikundi cha Vitabu vya Kiafrika (African Books Collective), kikundi kinachomilikiwa na kusimamiwa na wachapishaji wa Kiafrika. Mkuki na Nyota pia inashiriki na shirika zisizo za serikali (NGOs) kuimarisha kusoma na elimu Tanzania. Bgoya pia ni mwanzilishi wa Mtandao wa Wachapishaji wa Kiafrika (African Publishers Network) na alikuwa Mwenyekiti wa kamati ya kuamua ya Tuzo ya NOMA ya Uchapishaji Afrika (NOMA Award for Publishing in Africa). Walter Bgoya ametunga kazi nyingi za mada za kusoma, uandishi, uchapishaji na juhudi ya kutafuta sauti ya kweli ya Kiafrika katika dunia ya fasihi.
Chege Githiora ni Mhadhiri Mkuu wa Kiswahili katika Idara ya Lugha na Tamaduni za Kiafrika katika Chuo cha Masomo ya Maeneo ya Mashariki na Afrika (School of Oriental and African Studies), Chuo Kikuu cha London. Alizaliwa na kukulia Kenya na kusoma Meksiko na Marekani alikofundisha Kiswahili, lugha na fasihi, katika chuo cha El Colegio de Mexico, Chuo Kikuu cha Boston na Chuo Kikuu cha Michigan State alikohitimu na Shahada ya Uzamivu (PhD) katika Kugha mwaka wa 1999. Anaandika na kutafsiri kutoka na kwa Kikikuyu, Kiingereza, Kiwahili na Kihispania. Mada za utafiti na machapisho yake ni uzungumzaji wa lugha zaidi ya moja, tofauti kati ya lugha, misimu ya barobaro mijini, Kihispania na tamaduni na jamii mseto za Kiafrika na Kihispania, hati na utafsiri. Juu ya hayo, anafundisha na kutafiti muundo wa lugha za Kibantu hasa Kikikuyu na Kiswahili.
Sarit Shah ni mwenyekiti wa Mabati Rolling Mills Ltd,(MRM) moja ya kampuni zinazomilikiwa na kampuni ya Safal Group. Kwa bidhaa na vifaa vya ujenzi, kampuni ya MRM imekuwa tiba mujarab kwa kipindi cha miaka 60 katika mataifa ya Afrika. Mbali na hayo Sarit pia ni mwenyekiti wa wakfu wa Safal MRM, tawi linaloshughulika kutoa misaada la kampuni ya Safal Group. Wakfu wa Safal MRM umekuwa ukizisaidia jamii kwa zaidi ya miongo miwili katika nyanja za Elimu, Afya, Makazi na Mazingira.
Sarit amezuru mataifa ya Afrika na sasa yuko nchini Kenya ambapo anachangia pakubwa mikakati ya uongozi katika makundi ya kampuni za Safal. Ana ari katika masuala ya biashara endelevu na ustawi wa jamii. Aidha amechangia pakubwa mipango kadhaa ya elimu nchini Kenya kama vile, Taasisi ya Mafunzo ya Ufundi iliiyoko katika kaunti ya Kilifi. Taasisi hiyo hutoa mafunzo ya kiufundi kwa vijana 1000 kila mwaka kwa lengo la kuboresha viwango vyao vya kuajiriwa ama kujiajiri. Pamoja na hayo, Wakfu wa Safal MRM unaendesha kituo cha matibabu; Mabati Medical Centre, kinachotoa huduma bora za matibabu kwa zaidi ya wagonjwa 40000 nchini Kenya. Huduma zinazotolewa katika kituo hicho ni pamoja na; matunzo kamili ya afya, yakiwemo ushauri, matibabu, dawa na upimaji wa magonjwa kwa kutumia vifaa vya hali ya juu katika maabara. Kituo hicho pia hutoa tiba maalum kwa watu wenye matatizo ya macho, meno na huduma kwa wagonjwa wenye saratani ya mlango wa kizazi.
Ari ya Sarit kuhusu utamaduni, ilimchochea kufanikisha tuzo ya Fasihi ya Kiswahili barani Afrika ya Mabati-Cornell kwa miaka minane sasa. Tuzo hiyo inachangia maendeleo ya fasihi na elimu katika Afrika Mashariki, ambayo ni muhimu kwa utamaduni na ustawi wa jamii.
Sarit ana Shahada ya Sayansi katika masuala ya Uhandisi wa Umeme na vifaa meme kutoka Chuo Kikuu cha Uingereza na Shahada ya Uzamili kutoka Chuo Kikuu cha Rochester, New York, Marekani.
Ngugi wa Thiong’o anafundisha kwenye Idara za Fasihi Linganishi na Kiingereza kwenye Chuo Kikuu cha California, Irvine. Alizaliwa Kenya katika familia kubwa ya wakulima wadogo na kusomeshwa Shule za Msingi za Kamandura, Manguu na Kinyogori kisha Shule ya Upili ya Alliance, zote zilizoko Kenya. Kisha Chuo Kikuu cha Makerere (iliyokuwa chini ya Chuo Kikuu cha London wakati huo), Kampala, Uganda; na Chuo Kikuu cha Leeds, Uingereza. Amepokea Shahada za Uzamivu saba za Heshima. Mtaalamu wa aina kadhaa, yeye ni mwandishi wa riwaya, insha, michezo na habari, mhariri, msomi na mtetezi wa kuboresha jamii. Ngugi alipata kujulikana kwenye mandhari ya fasihi Afrika Mashariki kwa kuchezwa kwa mchezo wake mkuu wa kwanza, The Black Hermit (Mtawa Mweusi) kwenye Ukumbi wa Kitaifa wa Michezo Kampala. Aliandika Petals of Blood (Vijani vya Damu), Decolonizing the Mind (Ukombozi wa Akili) na vitabu vingine. Ni mshindi wa Tuzo ya Fasihi ya Lotusna Tuzo ya Kimataifa ya Nonino ya Fasihi: aliteuliwa kwa Tuzo ya Kimataifa ya Man Booker.Mwaka wa 2012, alituzwa Tuzo ya National Book Critics Award kwa In the House of the Interpreter (Nyumbani kwa Mtafsiri) pamoja na Nicolás Guillén Lifetime Achievement Award for Philiosophical Literature. Mwaka wa 2010 and 2014, alikuwa mmojawapo wa waandishi waliopendekezwa kwa Tuzo ya Nobel kwa Fasihi.
Clarissa Vierke
Ni professa wa fasihi ya lugha za kiafrika katika Chuo Kikuu cha Bayreuth, nchini Ujerumani. Yeye ni mpenzi wa lugha na fasihi za Kiswahili. Alianza kusaidia kuandaa Kongamano la Kiswahili la Bayreuth la kimataifa wakati alipokuwa bado mwanafunzi wa lugha na fasihi za Kiafrika zaidi ya miaka ishirini iliyopita, na bado analiendesha kila mwaka. Katika utafiti wake amejishughulisha haswa na na fasihi ya Kiswahili, hususan tenzi na mashairi za zamani zilizohifadhiwa kwa khati za Kiarabu. Hivi karibuni amefanya utafiti kuhusu miswada „iliyosafiri“ na inayopatikana pwani kote Afrika Mashariki, kama Kenya, Tanzania na vilevile Msumbiji. Pamoja na professa wengine wa fasihi ya kifaransa na fasihi linganishi anaendesha mradi wa utafiti kuhusu uhusiano wa kifasihi na kisanaa baina ya nchi mbalimbali na pande mbalimbali za bahari ya Hindi. Clarissa Vierke ni mtafiti mkuu wa “Cluster of Excellence Africa Multiple. Reconfiguring African Studies”, mradi mkuu wa utafiti unaofadhiliwa na serikali ya Ujerumani, na mwenyekiti wa jopo la “Ujumi na Sanaa” (“Arts and Aesthetics”). Pamoja na wenzake from Leipzig na Colgone nchini Ujerumani, Stellenbosch (Afrika Kusini), Wukari (Nigeria) na Eldoret (Kenya), alianzisha mradi wa “Recalibrating Afrikanistik” unaosaidiwa na Volkswagen Foundation na unaolenga kupanga masomo ya lugha na fasihi za Kiafrika kwa miaka ya mbele
Waakilishi zaidi watatangazwa