Mabati-Cornell Kiswahili Prize is featured on James Murua’s Literature Blog
Premium Times – Cornell university promotes African writing with a Prize
Kwa Matumizi ya Haraka!
Novemba 17, 2015
TUZO YA KISWAHILI YA MABATI-CORNELL
YA FASIHI YA KIAFRIKA
Tangazo la Washindi
Washindi wa tuzo mpya ya Mabati-Cornell ya Fasihi ya Kiafrika walitangazwa leo (10 Novemba 2015). Lengo kuu la tuzo hii ni kutambua uandishi bora kwa lugha za Kiafrika na kuhimiza tafsiri kutoka lugha za Kiafrika kwa lugha nyingine, baina ya lugha za Kiafrika zenyewe kwa zenyewe, na pia kwa lugha za Kiafrika.
Washindi wa kwanza wa tuzo hii ni:
Zawadi ya Kwanza ya Riwaya – $5,000: Anna Samwel kwa Penzi la Damu
Zawadi ya Kwanza ya Ushairi – $5,000: Mohammed K. Ghassani kwa N’na Kwetu
Zawadi ya Pili katika utanzu wowote – $3,000: Enock Maregesi kwa Kolonia Santita (riwaya)
Zawadi ya Tatu katika utanzu wowote, $2,000: Christopher Bundala Budebah kwa Kifaurongo (ushairi)
Hiyo ni miongoni mwa miswada 65 iliyowasilishwa, na kusomwa na waamuzi 6: Riwaya – Dk. Farouk Topan, Prof. Sheila Ryanga na Prof. Mohamed Bakari.
Ushairi – Bi. Rukiya Harith Swaleh, Prof. Clara Momanyi na Prof. Alamin Mazrui.
Waamuzi walisema kuwa, “ Wakitumia lugha inayovutia na iliyo muwafaka, na mara nyingine lugha cheshi, washindi walizungumzia maswala yanayozikumba jamii za Afrika Mashariki, kama vile utumiaji wa mihadharati na athari zake duniani; swala la jinsia – wanawake na haki zao; na ufisadi wa kisiasa. Huu ni ukweli halisi wa Afrika katika lugha ya Kiafrika.”
Washindi watakabidhiwa zawadi zao katika Tamasha la Fasihi la Kwani? (Kwani? Lit Fest) litakalofanyika Desemba 3, 2015 katika Klabu ya Capital mjini Nairobi, Kenya.
Sarit Shah, Mkurugenzi wa Mabati Rolling Mills Kenya alisema, “Kuongezeka kwa matumizi ya Kiswahili kuwa ni lugha kuu ya mawasiliano Afrika Mashariki hakuwezi kupuuzwa. Tunaamini kuwa lugha na tamaduni huboresha mahusiano ya kikazi na ya kibinafsi. Hapa Safal, hasa hapa Mabati, tunajivunia kuwa katika jamii hii inayoendelea kukua.”
Abdilatif Abdalla, Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini, alisema, “Jambo la kufurahisha ni kwamba sehemu kubwa ya miswada iliyopokewa ilikuwa ni ya kiwango cha juu. Kwa sababu ya kanuni za tuzo hii, ni washiriki wane tu ndio wanaoweza kutunukiwa zawadi. Hata hivyo, ni matumaini yangu kwamba hao washiriki wengine hawatavunjika moyo, bali wataendelea kushiriki katika mashindano yafuatayo, na kwamba baadhi yao watafarijika kwa maandishi yao kuchapishwa vitabu pia. Yanastahili.
Mjumbe wa Bodi ya Wadhamini, Ngugi Wa Thiong’o, alisema, “???
Mukoma Wa Ngugi, mwanzilishi-mwenzi wa tuzo hii alisema, “Kiwango cha msaada tuliopokea kinadhihirisha kuwa kuna uhitaji, na pia uwanja mpana wa kuandika kwa lugha za Kiafrika; na kuwa utamaduni wa Kiafrika wa fasihi unaweza kustawi katika lugha za Kiafrika, na kwamba lugha za Kiafrika zinaweza kukuzwa kupitia ufadhili kutoka Afrika kwenyewe.”
Lizzy Attree, mwanzilishi-mwenzi mwengine wa tuzo hii alisema, “Tunawashukuru wote walioleta miswada yao katika shindano hili, na tunatarajia kuwa tuzo ya mwaka huu itawahimiza waandishi zaidi kushiriki katika shindano la mwaka ujao.”
Masharti ya Tuzo:
- Tuzo itatolewa kwa muswada bora ambao bado haujachapishwa, au kwa kitabu kilichochapishwa miaka miwili kabla ya mwaka wa tuzo, katika tanzu za riwaya, tamthilia, ushairi, wasifu, na riwaya za michoro. Jumla ya dola za Marekani 15,000 zitatolewa zawadi kama ifuatavyo:
Zawadi ya Kwanza ya Riwaya – $5,000
Zawadi ya Kwanza ya Ushairi – $5,000
Zawadi ya Pili katika utanzu wowote – $3,000
Zawadi ya Tatu katika utanzu wowote – $2,000 - Kitabu au muswada utakaoshinda utachapishwa kwa Kiswahili na shirika la uchapishaji la East African Educational Publishers; na diwani bora ya mashairi itatafsiriwa na kuchapishwa na Africa Poetry Book Fund.
- Sherehe ya kuwatuza washindi wanne, itakayohudhuriwa na washindi wenyewe, itakuwa Kenya. Washindi hao wataalikwa Chuo Kikuu cha Cornell, watakakokuwa kwa wiki moja; kisha wiki moja nyingine watakuwa katika asasi shiriki (ya Marekani ama Afrika) mwaka 2016.
Shindano la mwaka 2016:
Washiriki wanaombwa kupeleka miswada ambayo haijachapishwa, au vitabu (riwaya, tamthilia, ushairi, wasifu, au riwaya za michoro), vilivyochapishwa kwa Kiswahili miaka miwili kabla ya mwaka wa tuzo, kwa: kiswahiliprize@cornell.edu kabla ya Machi 31, 2016. Miswada ya maandishi ya nathari isipungue maneno 50,000; na ya ushairi isipungue kurasa 60.
Waamuzi:
Waamuzi watabadilishwa kila mwaka na kuchaguliwa na wadhamini wa tuzo (TBA)
Tarehe Muhimu:
Tarehe ya mwisho ya kupeleka miswada au vitabu ni Machi 31, 2016. Orodha ya kwanza itatolewa Julai 2016, na washindi watatangazwa Oktoba 2016.
Kwa Wahariri:
Tuzo ya Kiswahili ya Mabati Cornell ya Fasihi ya Kiafrika ilianzishwa na Prof. Mukoma Wa Ngugi na Dk. Lizzy Attree mwaka wa 2014 ili kuendeleza uandishi bora kwa lugha za Kiafrika na kuhimiza tafsiri kutoka lugha za Kiafrika kwa lugha nyingine, pia baina ya lugha za Kiafrika zenyewe kwa zenyewe.
Tuzo ya Mabati-Cornell:
Kwa kiasi kikubwa, tuzo hii inadhaminiwa na Mabati Rolling Mills of Kenya (sehemu ya Kampuni ya Safal), Ofisi ya Makamu wa Mkuu wa Maswala ya Kimataifa katika Chuo Kikuu cha Cornell, Idara ya Masomo na Utafiti ya Afrikana
Mabati Rolling Mills:
Mabati ni sehemu ya Kampuni ya Safal, inayotengeneza mabati katika nchi 11 za Mashariki ya Afrika na Kusini mwa Afrika.
www.safalgroup.com
Ofisi ya Makamu wa Mkuu wa Maswala ya Kimataifa katika Chuo Kikuu cha Cornell inatoa mwongozo na kusaidia katika kusimamia juhudi za kuzidisha shughuli za kimataifa Cornell. Lengo lake ni kushirikiana na shule, vyuo na vituo ili kuendeleza na kutekeleza mipango inayohusiana na shughuli za kimataifa za Chuo Kikuu hiki. Ofisi hii itaisaidia Halmashauri mpya ya Kimataifa, ambayo mwenyekiti wake ni Makamu wa Mkuu.
http://international.cornell.edu/international_vision
Idara ya Masomo na Utafiti ya Afrikana Idara ya Masomo na Utafiti ya Afrikana mazingira ya kielimu, ya kitamaduni na ya kijamii kwenye Chuo Kikuu cha Cornell, Ithaca. Tovuti:
http://www.asrc.cornell.edu
East African Educational Publisher (EAEP) ni shirika mojawapo kuu la wachapishaji. EAEP linajitahidi kuyahusisha maadili yanayoonekana kama kwamba yanakinzana; yaani kuchapisha kazi za kiwango cha juu zinazogusia maswala ya kijamii, ya kitamaduni na ya kiuchumi, na wakati huo huo kufaulu kufanya biashara iliyo tayari kukabiliana na hali halisi na misukosuko ya zama za kiteknolojia. Tovuti: http://www.eastafricanpublishers.com
Africa Poetry Book Fund inaimarisha na kuendeleza uchapishaji wa sanaa za kishairi kupitia vitabu vyake, mashindano, warsha na semina pamoja na kushirikiana na wachapishaji, matamasha, mawakala, vyuo, vyuo vikuu, makongamano na vikundi vingine vinavyohusika na ushairi Afrika. Wovuti: http://africanpoetrybf.unl.edu/
Wadhamini: Abdilatif Abdalla (Mwenyekiti), Mukoma wa Ngugi, Lizzy Attree, Happiness Bulugu, Walter Bgoya, Henry Chakava, Chege Githiora, Carole Boyce Davies, Rajeev Shah, Ngugi Wa Thiong’o – na wengine watakaotangazwa baadaye.
Tovuti: http://blogs.cornell.edu/kiswahiliprize/
Twitter: @KiswahiliPrize
Facebook: https://www.facebook.com/pages/Mabati-Cornell-Kiswahili-Prize-for-African-Literature/1534905843433822
Kwa Mawasiliano:
Prof. Mukoma Wa Ngugi, kiswahiliprize@cornell.edu
Dr Lizzy Attree, kiswahiliprize@cornell.edu
CHUO KIKUU CHA CORNELL, SHULE YA SANAA NA SAYANSI
KWA UTANGULIZI WA HIMA
Novemba 21, 2014
Tuzo Kuu Mpya ya Fasihi ya Kiafrika Yatangazwa
ITHACA, NY. – Tuzo mpya ya Kiswahili ya Mabati Cornell ya Fasihi ya Kiafrika ilitangazwa leo Nigeria kwenye tamasha ya Ake Art & Books iliyokuwa Abeokuta. Tuzo hii ni inatambua uandishi bora katika lugha za Kiafrika na kuhimiza utafsiri kutoka, kati na kwa lugha za Kiafrika.
Mwandishi mashuhuri Ngugi Wa Thiong’o aliamba “Tuzo ya Mabati-Cornell ni utatuzi mkubwa katika kupigania uandishi katika lugha za kiafrika, kupata nafasi yao ya kuonekana kwenye jua la dunia ya fasihi. Kwa ujumla, tuzo zimetumika kuzamisha fasihi ya Kiafrika katika lugha za Kiafrika kwenye mafuriko ya lugha za Ulaya. Na tuzo ya Mabati-Cornell, ndoto za Diop, A.C Jordan, Obi Wali na wengine zi hai. Natumai tuzo hii itakuwa mwaliko kwa lugha zingine za kiafrika kufanya hivi hivi na zaidi.”
Zaidi ya watu milioni 140 wanazungumza Kiswahili katika Afrika Mashariki na Kusini; Kiswahili pia ni lugha rasmi Kenya na Tanzania. Tuzo itatolewa kwa nakala bora ambayo haijachapishwa bado au kitabu kilichochapishwa katika miaka miwili kabla ya mwaka wa tuzo katika tanzu za ngano, ushairi na wasifu, na riwaya Washindi wa kwanza katika tanzu za riwaya na ushairi watapokea $5,000; tuzo ya nafasi ya pili katika utanzu wowote ni $3,000 na tuzo ya nafasi ya tatu ni $2000.
Kitabu au nakala itakayoshinda itachapishwa katika Kiswahili na Wachapishaji wa Kielimu wa Afrika Mashariki (East African Educational Publishers) na diwani ya mashairi bora itatafsiriwa na kuchapishwa na Akiba ya Afrika ya Ushairi (Africa Poetry Book Fund). Tamasha ya kutoa tuzo zitakuwa Chuo Kikuu cha Cornell, Kenya na Tanzania. Waandishi wanne waliotuzwa wataketi Chuo Kikuu cha Cornell kwa wiki moja kisha wiki moja zaidi katika taasisi inayoshiriki.
Profesa wa Kiingereza Cornell, Mukoma Wa Ngugi, mmojawapo wa waanzilishi wa tuzo, alisema kwamba “tuzo inatambua kuwa lugha zote ziliumbwa sawa na hakuna lugha inayofaa kufaulu kwa gharama ya lugha nyingine. Fauka ya utambulisho huo, tuzo hii inatoa mfano kihistoria wa ufadhili kwa Afrika kutoka Waafrika na kuonyesha kuwa hisani ya Kiafrika inaweza na inafaa kuwa kiini cha utungaji wa sanaa za kitamaduni za Kiafrika.”
Sarit Shah, Mkurugenzi wa Mabati Rolling Mills Kenya alisema “Kuimarisha fasihi na ujuzi wa kusoma na kuandika ni muhimu kwa kuendeleza utamaduni stawi, na Mabati Rolling Mills ina furaha kusaidia kifedha katika kuanzisha mradi mpya wa kuchapisha lugha za Kiafrika. Tuzo mpya ya fasihi ya Kiswahili inanuia kuwatuza waandishi wasanii na wataalamu wa Afrika Mashariki, wanaotumia kazi zao kuhimiza kuandika na kusoma katika matabaka yote ya jamii. Tunaamini kuwa ni muhimu kulinganisha dunia ya mawazo na ile ya vitendo kama biashara na uchumi.”
Mhakiki wa fasihi, Lizzy Attree, mwanzilishi mwengine wa tuzo mpya alisema “Licha ya kuwepo na tuzo za fasihi za Kiafrika kama tuzo ya Caine na Etisalat iliyoanzishwa karibuni, hakuna tuzo kubwa ya kimataifa na Kiafrika zinazotunuku fasihi zilizotungwa katika lugha za Kiafrika. Tuzo ya Mabati-Cornell ya fasihi ya Kiafrika inachangia pakuu kwa fasihi duniani, kuanzisha tuzo hii mpya inatoa mfano kwa fasihi katika lugha zingine za Kiafrika.”
Laurie Damiani, Mkurugenzi wa miradi ya kimataifa katika Chuo Kikuu cha Cornell kwenye Ofisi ya Makamu wa Provost wa Masuala ya Kimataifa alisema kuwa wana furaha kuwa wadhamini wa mradi huu unaosisimua na unaoingiliana na jinsi Cornell inathamini umataifa wa jamii. Alisema “Ni staha kubwa kushiriki katika juhudi za kuimarisha tamaduni za fasihi zinazosisimua na kuhimiza kuingiliana kati ya watu wa Afrika Mashariki.”
Wadhamini wakuu wa tuzo hii ni Mabati Rolling Mill wa Kenya (sehemu ya Kikundi cha Safal). Ofisi ya Makamu wa Provost wa Masuala ya Kimataifa Chuko Kikuu cha Cornell na Idara ya Masomo ya Afrikana Chuo Kikuu cha Cornell.
Kwa Habari Zaidi: http://kiswahiliprize.cornell.edu
Anwani ya Twitter: @KiswahiliPrize
Habari za Wakala:
Prof. Mukoma Wa Ngugi, kiswahiliprize@cornell.edu
Dr Lizzy Attree, kiswahiliprize@cornell.edu