Waamuzi

TUZO YA KISWAHILI  YA MABATI-CORNELL YA

FASIHI YA AFRIKA

Tangazo la Majaji 2021

Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini ya Tuzo ya Kiswahili ya Mabati-Cornell ya Fasihi ya Afrika, Abdilatif Abdalla. amewatangaza Majaji wa mwaka 2021 kuwa ni Prof. Aldin K. Mutembei, Dkt. Salma Omar Hamad na Dkt. Joseph N. Maitaria. Mwenyekiti wa Bodi alitangaza pia kwamba  Prof. Rocha Chimerah na Dkt. Hamisi Babusa watakuwa majaji wa Tuzo ya Nyabola, tuzo maalumu ya mwaka 2021 kwa vijana wenye umri wa baina ya  miaka  18 na 35 walioandika hadithi za kubuni za  kisayansi na  kidhana.

“Mwaka huu wa 2021 Tuzo imeshuhudia ongezeko la idadi kubwa ya washiriki ambayo haikutarajiwa – kutoka washiriki 96 mwaka 2019 hadi 256. Vile vile, miswada tuliyoipokea mwaka huu ilitoka nchi 13 na sehemu mbalimbali ulimwenguni: Tanzania, Kenya, Uganda, Burundi, Misri, Nigeria, Marekani, Kanada, Ujerumani, Austria, Uswisi, Finland, na Uholanzi. Tunafurahi sana kuona kwamba sura ya umajumui wa Afrika wa Tuzo hii imevuka mipaka ya bara la Afrika,” amesema Munyao Kilolo, msimamizi wa Tuzo.

Na Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini, Abdilatif Abdalla, amesema, “Ni furaha kuu ilioje kuona jinsi washiriki wanavyoongezeka, na pia kuona viwango vya maandishi yanayoletwa kwenye mashindano vikipanda juu kila Tuzo hii inavyoendelea kupata umaarufu na kuwafanya Waafrika kutoka sehemu mbalimbali duniani kushiriki. Ni matumaini yetu kwamba Tuzo hii hatimaye itasaidia katika kulitimiza lengo la Umajumui wa Afrika, ambalo tumekuwa na hamu nalo kwa miaka mingi. Pia nataka kuwahimiza waandishi wanawake washiriki kwenye mashindano ya Tuzo hii kwa idadi kubwa ili kulipunguza hili pengo la kijinsia lililoko hivi sasa.”

Mwanzilishi wa Tuzo Maalumu ya Nyabola, Bi Nanjala Nyabola amesema, “Ni muhimu sana kwamba jamii zinazozungumza Kiswahili zinaendela kuhusika na ubunifu na utumizi wa maneno au maendeleo mapya yanayohusu teknolojia,” aliongeza Nyabola, “na hakuna harakati bora zaidi ya kuendeleza kazi hii ila kwa kuunga mkono uandishi bora kuhusu sayansi na teknolojia”.

Wakishaisoma na kuitathmini miswada iliyotimiza vigezo vya  mashindano haya, Majaji watawachagua washiriki watakaoingia katika orodha fupi, ambayo itatangazwa Novemba mwaka huu. Washindi wa kila kitengo watakaofaulu kuingia kwenye orodha ya mwisho ya watatangazwa kwenye sherehe ya kuwatunuku washindi zawadi zao, ambayo mwaka huu itafanyika Dar es Salaam, Tanzania, katikati ya Desemba.

Baada ya kuyasitisha mashindano ya mwaka 2020 kutokana na kuzuka kwa janga la UVIKO-19, waanzilishi wa tuzo, Dkt. Lizzy Attree na Prof. Mukoma Wa Ngugi, wamefurahishwa kuona mwaka huu mashindano yamerudi tena kwa nguvu mpya. Ukuaji wa Tuzo hii ni mfano mzuri wa kuzitia moyo tuzo nyengine za maandishi kwa lugha za Afrika.

Tuzo ya Kiswahili ya Mabati Cornell ya Fasihi ya Afrika ilianzishwa mwaka 2014 ili kuimarisha uandishi kwa lugha za Afrika na kuhimiza tafsiri kutoka lugha hizo, baina ya lugha hizo zenyewe kwa zenyewe, na kwa lugha hizo.

Majaji wa 2021

Prof. Aldin K. MutembeiProf. Aldin K. Mutembei (Shahada ya Kwanza (Elimu).; Shahada ya Uzamili (Isimu) (Dar); Shahada ya Uzamili (Fasihi); Shahada ya Uzamivu (Leiden) ni Mgoda, Kigoda cha Uprofesa wa Kiswahili cha Mwalimu Julius Nyerere, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. Kabla ya hapo alikuwa Mkurugenzi wa Taasisi ya Taaluma za Kiswahili; na sasa ni Mkurugenzi wa Taasisi ya Confucius, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. Anasomesha Fasihi ya Kiswahili/Kiafrika, Mawasiliano, Nadharia za Uhakiki, Fasihi Simulizi na Lugha ya Kiswahili kwa wazungumzaji wa lugha nyengine. Ameshachapisha vitabu vine, miongoni mwa hivyo ni riwaya Kisiki Kikavu (E & D Limited, 2005) na Korasi Katika Fasihi: Nadharia Mpya ya Uhakiki (Taasisi ya Taaluma za Kiswahili, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, 2012).

Dkt. Salma Omar Hamad Dkt. Salma Omar Hamad alizaliwa Pemba, Zanzibar, mwaka 1980. Hivi sasa ni Mhadhiri wa Fasihi ya Kiswahili na Isimu katika Chuo Kikuu Huria cha Tanzania. Alipata shahada yake ya kwanza ya Kiswahili (Elimu) kutoka Chuo Kikuu cha Taifa Zanzibar (SUZA); na Shahada ya Uzamili (Isimu) kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Shahada yake ya Uzamivu  katika Kiswahili aliipata kutoka Chuo Kikuu cha Taifa Zanzibar. Dkt. Salma ameandika hadithi fupi kadhaa zilizoko kwa wachapishaji zikisubiri kuchapishwa. Pia amechangia hadithi katika mikusanyo ya hadithi fupi; kama vile hadithi yake, “Shibe Inatumaliza” kwenye mkusanyo uitwao Tumbo Lisiloshiba na Hadithi Nyingine (Longhorn Publishers, 2016).

Dkt. Joseph N. MaitariaDkt. Joseph N. Maitaria ni Mhadhiri Mwandamizi na Mkuu wa Idara ya Sanaa na Lugha, Kitivo cha Elimu na Sayansi za Kijamii, Chuo Kikuu cha Karatina, Kenya. Ana shahada ya Kwanza ya Ualimu (Chuo Kikuu cha Kenyatta) ambapo alisomea Shahada ya Elimu, Kiswahili na Dini. Shahada ya Uzamili alisomea Fasihi ya Kiswahili (Chuo Kikuu cha Kenyatta), na Shahada ya Uzamivu kuhusu Ushairi wa Kiswahili (Chuo Kikuu cha Kenyatta). Yeye pia ni mwanachama na Katibu wa vyama vya kitaaluma vya Kiswahili, kama vile Chama cha Kiswahili cha Afrika Mashariki (CHAKAMA) na Chama cha Kiswahili cha Taifa (CHAKITA), Kenya. Dkt. Maitaria amechapisha vitabu na makala kadhaa kuhusu Fasihi ya  Kiswahili kwenye majarida ya kitaaluma.

Dkt. Hamisi BabusaDkt. Hamisi Babusa ni Mhadhiri wa Kiswahili na Taaluma ya Ufundishaji Lugha, Chuo Kikuu cha Kenyatta, na kwa sasa ni Mkuu wa Kitengo. Miongoni mwa vyuo vikuu alivyosomesha ni

Chuo Kikuu cha St. Lawrence, Marekani. Dkt. Babusa pia ni mwandishi wa kazi za kibunifu na za kitaaluma, miongoni mwa hizo ni Kamusi Teule, ambayo ni kamusi ya methali za Kiswahili na visawe vyake kwa Kiingereza. Amechangia pia katika mikusanyo mbalimbali ya mashairi na hadithi fupi. Pia ameandika vitabu vya watoto, kama vile mfululizo wa Binti Kitabu na wa Makumba, ambazo ni hadithi za kubuni za kisayansi na kidhana. Hadithi hizo zilimfanya kutambuliwa kuwa ni miongoni mwa wanasayansi 20 bora Kenya kwa mwaka 2018.

Prof. Rocha ChimerahProf. Rocha Chimerah ni Profesa wa Isimu ya Kiswahili katika Chuo Kikuu cha Pwani, Kilifi, Kenya. Alihitimu shahada yake ya uzamivu mwaka 1989, Chuo Kikuu cha Ohio, Marekani. Alisomesha Rwanda kwa miaka minane, na amechapisha makala kadha wa kadha kuhusu Lugha na Fasihi ya Kiswahili katika majarida ya kitaaluma ya Afrika Mashariki na ya nchi za nje. Miongoni mwa riwaya zake zilizochapishwa ni Nyongo Mkalia Ini na Siri Sirini (juzuu tatu), kadhalika na tamthilia. Mwaka 2000 alitunukiwa Tuzo ya Noma kwa kitabu alichoshiriki kukiandika, Ufundishaji wa Fasihi: Nadharia na Mbinu. Kitabu chake kingine,  Kiswahili: Past, Present and Future Horizon kiliorodheshwa na Tamasha la Vitabu, Harare, Zimbabwe, mwaka 2002 kuwa ni miongoni mwa Vitabu Bora 100 vya Afrika vya Karne ya 20.

Kwa Wahariri: 

Tuzo ya Kiswahili ya Mabati-Cornell ya Fasihi ya Kiafrika, yenye thamani ya jumla ya Dola za Marekani 15,000, hutolewa kila mwaka kwa miswada bora, au kwa vitabu vilivyochapishwa miaka miwili kabla ya mwaka wa kutolewa zawadi, katika fani za riwaya, ushairi, mkusanyo wa hadithi fupi, riwaya za picha na wasifu. Miswada inayoshinda huchapishwa na mashirika ya uchapishaji vitabu, Mkuki na Nyota Publishers na East African Educational Publishers (EAEP). Na mswada bora wa ushairi hufasiriwa kwa Kiingereza na kuchapishwa kitabu na shirika la Africa Poetry Book Fund.

Tuzo hii inadhaminiwa na kampuni ya Mabati Rolling Mills, Kenya, na kampuni ya ALAF Limited, Tanzania (ambazo ni miongoni mwa kampuni za Safal Mauritius Limited); pia na Ofisi ya Makamu wa Mkuu wa Maswala ya Kimataifa katika Chuo Kikuu cha Cornell, Idara ya Taaluma za Afrika ya Chuo Kikuu cha Cornell, Marekani, na Wakfu wa Ngugi wa Thiong’o (Ngugi wa Thiong’o Foundation).

Kampuni ya Safal Investments Mauritius Limited na matawi yake (ambayo ni pamoja na Mabati Rolling Mills Limited, Kenya, na ALAF Limited, Tanzania) inajulikana kwa jina la jumla la The Safal Group. Hii ni kampuni kubwa kabisa inayotengeneza mabati katika nchi 12 za Afrika. www.safalgroup.com

Mabati Rolling Mills Limited (MRM) ilibuniwa zaidi ya miaka 50 iliyopita. Ni kampuni kubwa kabisa Kenya inayotengeneza mabati ya kuezekea mapaa, na inaongoza katika utanzu huu wa ufundi. Pia inaongoza katika bara la Afrika kwa kutengeneza mabati ikitumia teknolojia ya hali ya juu kabisa inayopatikana duniani. Mabati yake maarufu yanasifika na yanaaminiwa na mamilioni ya wajenzi. www.mabati.com

Safal MRM Foundation, yenye makao yake Kenya, ni kitengo cha Mabati Rolling Mills na Safal Group kinachoshughulika na kutoa misaada ya aina mbalimbali. Miongoni mwa misaada hiyo, inayotolewa Mariakani, Kenya, ni kuanzisha na kuendelea kugharimia uendeshaji wa Taasisi ya Mabati ya Mafunzo ya Teknolojia (Mabati Technical Training Institute), na Kituo cha Mabati cha Matibabu (Mabati Medical Centre). www.safalmrmfoundation.org

ALAF Limited (ALAF) ni kampuni ya Tanzania inayoongoza katika utengenezaji wa mabati ya kuezekea mapaa. Tangu ilipobuniwa mwaka 1960, ALAF imeendelea kuchangia kwa kiasi kikubwa katika shughuli za ujenzi nchini. ALAF haitengenezi mabati ya kuezekea mapaa tu, bali pia aina za nyaya za chuma zinazotumika katika ujenzi wa mapaa. ALAF pia inatengeneza mabomba ya metali yanayotumika katika shughuli mbalimbali za ufundi. www.alaf.co.tz

Ofisi ya Makamu wa Mkuu wa Maswala ya Kimataifa katika Chuo Kikuu cha Cornell inatoa mwongozo na kusaidia kusimamia juhudi za kuzidisha shughuli za kimataifa Cornell. Lengo lake ni kushirikiana na shule, vyuo na taasisi nyengine ili kuendeleza na kutekeleza mipango inayohusiana na shughuli za kimataifa za Chuo Kikuu hiki. Ofisi hii inaisaidia Halmashauri mpya ya Kimataifa, ambayo mwenyekiti wake ni Makamu wa Mkuu. http://international.cornell.edu/international_vision

Idara ya Taaluma za Afrika na Utafiti inachangia kwa kiasi kikubwa katika shughuli za kitaaluma, kitamaduni na za kijamii kwenye Chuo Kikuu cha Cornell, Ithaca. http://www.asrc.cornell.edu

Ngugi Wa Thiong’o Foundation Wakfu huu unapata nguvu zake kutokana na hamu  na ari ya kukuza kuonekana kwa Lugha za Kiafrika nchini Kenya, barani Afrika, na duniani, na kutambuliwa kuwa ni vyombo mwafaka vya kuendeshea shughuli za sanaa ya uigizaji, ubunifu, uvumbuzi, na taaluma. Pia unazitambua lugha hizi kwamba zina uwezo wa kuwa mstari wa mbele katika kila fani – tangu utamaduni, sayansi za kibiolojia, teknolojia hadi tiba.   http://ngugiwathiongofoundation.org

East African Educational Publisher (EAEP) ni shirika mojawapo kuu la wachapishaji. EAEP linajitahidi kuyahusisha maadili yanayoonekana kama kwamba yanakinzana; yaani kuchapisha kazi za kiwango cha juu zinazogusia maswala ya kijamii, ya kitamaduni na ya kiuchumi, na wakati huo huo kufaulu kufanya biashara iliyo tayari kukabiliana na hali halisi na misukosuko ya zama za kiteknolojia. Mwaka  2016 shirika hili lilichapisha riwaya Penzi la Damu, ya Anna S. Manyanza, iliyoshinda nafasi ya kwanza mwaka huo, na riwaya Kolonia Santita, ya Enock Maregesi, iliyoshinda nafasi ya pili. http://www.eastafricanpublishers.com

Mkuki na Nyota Publishers ni shirika huru la uchapishaji vitabu vya kimaendeleo, kiukombozi, vya bei nafuu na maridadi. Shirika hili lilianzishwa mwaka 1991 kutokana na ukosefu wa vitabu vya kiwango cha juu nchini Tanzania. Kaulimbiu yake ni kuchapisha “Vitabu Vinavyofaa, Vitabu vya Bei Nafuu, na Vitabu Maridadi.” Disemba 2018 shirika hili liliichapisha diwani ya mshairi Dotto Rangimoto, Mwanangu Rudi Nyumbani, iliyoshinda nafasi ya kwanza ya ushairi katika mashindano haya ya mwaka 2017. Na mwezi wa Januari 2019 likaichapisha riwaya ya Ali Hilal Ali, Mmeza Fupa, iliyoshinda nafasi ya kwanza ya mashindano haya katika sehemu ya riwaya, mwaka 2017. http://www.mkukinanyota.com

Africa Poetry Book Fund inaimarisha na kuendeleza uchapishaji wa sanaa za kishairi kupitia vitabu vyake, mashindano, warsha, semina, pamoja na kushirikiana na wachapishaji, matamasha, mawakala, vyuo, vyuo vikuu, makongamano, na vikundi vingine vinavyohusika na ushairi Afrika. http://africanpoetrybf.unl.edu/

Bodi ya Wadhamini: Abdilatif Abdalla (Chair), Mukoma wa Ngugi, Lizzy Attree, Happiness Bulugu, Walter Bgoya, Henry Chakava, Chege Githiora, Clarissa Vierke, Farouk Topan, Carole Boyce Davies, and Ngugi Wa Thiong’o.

Msimamizi (Administrator): Moses Kilolo

Tofuti: http://blogs.cornell.edu/kiswahiliprize/

Twitter: @KiswahiliPrize

Facebook: https://www.facebook.com/pages/Mabati-Cornell-Kiswahili-Prize-for-African-Literature/1534905843433822

Kwa mawasiliano zaidi:  Prof. Mukoma Wa Ngugi, Cornell University, kiswahiliprize@cornell.edu, Dr Lizzy Attree, kiswahiliprize@cornell.edu, Munyao Kilolo  kiswahiliprize@cornell.edu.

Majaji wa 2019

Prof. Clara Momanyi ni Mkenya ambaye amefunza Fasihi ya Kiswahili katika vyuo vikuu vya Kenya kwa zaidi ya miaka 20. Tasnifu yake ya uzamili ilikuwa ni kuhusu Fasihi ya Kiswahili na Maswala ya Jinsia. Pia ni mwandishi wa riwaya, hadithi fupi na mashairi. Miongoni mwa vitabu vyake ni Ushindi wa Nakate, kitabu cha hadithi kilichoshinda tuzo ya Jomo Kenyatta-Textbook Centre Prize for Literature, mwaka wa 2015, katika kitengo cha fasihi ya watoto.  Vitabu vyake vyengine ni pamoja na TumainiNakuruto na Pendo Katika Shari.

Maandishi yake ya kitaaluma yamechapishwa katika majarida mbalimbali yanayotambulika. Kwa sasa Prof. Momanyi anajishughulisha zaidi na utafiti katika Fasihi ya Kiswahili, pamoja na kutafsiri kwa Kiswahili nyaraka mbalimbali za kitaifa na za kimataifa kutoka Kiingereza.

Mwaka wa 2015 Prof. Momanyi alikuwa mmojawapo wa majaji wa  shindano la kwanza la Tuzo ya Kiswahili ya Mabati-Cornell ya Fasihi ya Afrika. Pia amekuwa jaji katika mashindano ya Tuzo nyengine kadhaa za Fasihi ya Kiswahili, kwa mfano Jomo Kenyatta Prize for Literature, Kenya, ambapo alishiriki kuteua kazi bora za fasihi katika Kiingereza na Kiswahili.

 

Ahmed Rajab, mzawa wa Zanzibar, ni mwandishi wa kimataifa, mchambuzi wa siasa, mwandishi wa insha na mwanasahafu wa Raia Mwema gazeti kubwa la kila wiki la Tanzania. Ana shahada ya Falsafa kutoka Chuo Kikuu cha London, stashahada ya juu katika Taaluma ya Miji ya Nchi Zinazoendelea kutoka chuo cha University College, London, na shahada ya uzamili katika somo la Fasihi ya Kisasa ya Kiafrika kutoka Chuo Kikuu cha Sussex. Tasnifu yake ilikuwa juu ya David Diop, mshairi wa falsafa ya Négritude.

Ahmed amewahi kufanya kazi katika Idhaa ya BBC, jarida la Index-on-Censorship, gazeti la Africa Events, jarida la Africa Analysis, pamoja na kwenye mashirika ya Umoja wa Mataifa ya Unesco na UNDP. Kutoka 2006 hadi 2009 alikuwa Mkuu wa Chumba cha Habari, Dubai, (akisimamia eneo la Mashariki ya Kati na Asia) katika Shirika la Habari za Kibinadamu la IRIN, lililokuwa chini ya Umoja wa Mataifa. Baadaye aliishi Nairobi kwa miaka mitatu akiwa Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni ya televisheni ya Universal TV.  Siku hizi anafanya kazi ya kutoa ushauri na ni mshiriki wa Taasisi ya Gusau iliyoko Kaduna, Nigeria. Baadhi ya mashairi ya Ahmed yamo kwenye kitabu cha mkusanyiko wa mashairi kiitwacho African New Voices, kilichochapishwa na Longman mwaka 1997. Amefasiri kwa Kiswahili vitabu viwili vya watoto vilivyochapishwa karibuni na wachapishaji wa Salaam Publishing, jijini London.  Mwaka 2018 Ahmed Rajab alikuwa mmojawapo wa majaji wa Tuzo ya Caine ya Uandishi wa Kiafrika.

 

Dkt. Amiri Swaleh ni Mhadhiri Mwandamizi katika Idara ya Kiswahili, Chuo Kikuu cha Nairobi; na amekuwa akisomesha Fasihi ya Kiswahili na Isimujamii kwa miaka 27 sasa. Kwa hivi sasa ni Mkuu wa Kitengo cha Fasihi katika Idara ya Kiswahili. Mbali na makala yake ya kitaaluma yaliyochapishwa katika majarida mbalimbali, vile vile Dkt. Amiri ni mwandishi wa hadithi fupi ambazo zimechapishwa katika mikusanyo ya hadithi fupi, kama vile Kosa la Nani? na Hadithi Nyingine (2018).

Nyanja za kitaaluma anazoshughulika nazo zaidi ni pamoja na utafiti, uhakiki na uchambuzi wa Fasihi ya Kiswahili, hasa katika vipengee vya maswala ya kijinsia, ushairi wa Kiswahili wa kale, historia ya Kiswahili, lugha na maendeleo ya jamii, na mifumo ya kisiasa

 

Skip to toolbar