Washindi wa mwaka 2017 ni

Riwaya

 • Ally Hilal

Ali Hilal Ali ni mwandishi chipukizi wa riwaya na mashairi ya Kiswahili. Alizaliwa kijiji cha Kalani, Pemba, mwaka 1989, na kukulia katika mji wa Wete Pemba, Zanzibar. Alianza masomo yake mwaka 1997 katika Shule ya Msingi ya Jadida, Wete, Pemba; na masomo ya sekondari kuanzia mwaka 2004 katika Chuo cha Kiislamu, Kiuyu, Micheweni, Pemba. Baada ya hapo akaendelea na masomo katika Chuo cha Usimamizi wa Fedha (IFM), Dar es Salaam, ambapo mwaka 2013 alihitimu Shahada ya Kwanza katika Sayansi ya Hifadhi ya Jamii (BSc in Social Protection).

Alianza kujishughulisha na kuandika riwaya na mashairi mwaka 2008. Riwaya yake ya kwanza, Safari Yangu, ilichapishwa na Buluu Publishing, Ufaransa, mwaka 2015. Pia amechangia mashairi kadhaa kwenye Diwani ya Kurasa Mpya, ambayo ni mkusanyo wa mashairi ya washairi watano.

Email: ahbenylal7@gmail.com

Ushairi

 • Dotto Rangimoto

Dotto Rangimoto alizaliwa Morogoro, Tanzania, mwaka 1986. Baada ya kupata elimu ya sekondari katika Shule ya Sekondari ya Morogoro, mwaka 2004, Dotto amekuwa akijishughulisha na biashara ndogondogo na kilimo. Yeye ni mpenzi mkubwa wa Fasihi ya Kiswahili, hasa hadithi na mashairi; na ni miongoni mwa washairi chipukizi wa Kiswahili.

Email: mzalendo.njano5@gmail.com

__________________________________________________________________________________________________________________________________

Kama ilivyotangazwa kabla, wafuatao ni waandishi wengine waliokuwamo katika orodha fupi:

 • Ally Hilal (Tanzania), Mmeza Fupa (riwaya)
 • Hussein Wamaywa (Tanzania), Mkakati wa Kuelekea Ikulu (riwaya)
 • Richard Atuti Nyabuya (Kenya), Umalenga wa Nyanda za Juu (ushairi)

Maandishi hayo ni miongoni mwa miswada 20 iliyosomwa na waamuzi watatu:

 • Prof. Rayya Timammy – Profesa Mshiriki, Idara ya Kiswahili, Chuo Kikuu cha Nairobi
 • Dkt. Shani Omari – Mhadhiri Mwandamizi, Idara ya Fasihi, Mawasiliano na Uchapishaji, Taasisi ya Taaluma za Kiswahili, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam
 • Prof. Joshua S. Madumulla – Profesa Mshiriki wa Fasihi, Chuo Kikuu cha Tumaini, Iringa

Wakizingatia historia ndefu ya fasihi ya Kiswahili, waamuzi walisema, “Kwenye riwaya iliyopata ushindi wa kwanza, swala la mwanamke limejadiliwa kwa urefu. Mwanamke amewakilishwa katika nyanja na nafasi zake mbalimbali katika jamii. Mila na desturi zinazotumiwa kumkandamiza mwanamke zimedhihirishwa kuwa ni miongoni mwa vikwazo vikubwa vinavyomzuia mwanamke kuendelea na kufanikiwa. Lakini mwanamke anapambana dhidi ya vikwazo hivyo na, hatimaye, anafaulu.”

Mashairi yaliyomo katika muswada ulioshinda yametungwa kwa lahaja ya Kimvita, inayozungumzwa Mombasa. Lahaja hii imetumiwa na washairi maarufu wa nyakati mbalimbali katika historia; kwa mfano Muyaka wa Muhaji, mshairi mashuhuri wa karne ya 19. Pia imetumiwa na washairi wa wakati wetu huu: Ahmad Nassir Juma Bhalo, Abdilatif Abdalla, na sasa Ahmed Hussein Ahmed. Hii ni lahaja iliyo na utajiri mkubwa wa msamiati  na sauti mbalimbali za matamshi ya maneno.”

Mwaka huu, zawadi za Tuzo hii zitatolewa Tanzania katika Hoteli ya Hyatt Regency Dar es Salaam, Kilimanjaro, Ukumbi wa Kibo, tarehe 16 Januari, 2017.

Kwa Wahariri:

Tuzo ya Kiswahili ya Mabati-Cornell ya Fasihi ya Kiafrika, yenye thamani ya jumla ya Dola za Marekani 15,000, hutolewa kila mwaka kwa miswada bora, au kwa vitabu vilivyochapishwa miaka miwili kabla ya mwaka wa kutolewa zawadi, katika fani za riwaya, ushairi, wasifu na riwaya za picha. Miswada inayoshinda huchapishwa na shirika la uchapishaji vitabu la East African Educational Publishers (EAEP). Na mswada bora wa ushairi hufasiriwa kwa Kiingereza na kuchapishwa kitabu na shirika la Africa Poetry Book Fund.

Tuzo hii inadhaminiwa na kampuni ya Mabati Rolling Mills, Kenya, na kampuni ya ALAF Limited, Tanzania (ambazo ni miongoni mwa kampuni za Safal Mauritius Limited); pia na Ofisi ya Makamu wa Mkuu wa Maswala ya Kimataifa katika Chuo Kikuu cha Cornell, na Idara ya Taaluma za Afrika ya Chuo Kikuu cha Cornell, Marekani.

Kampuni ya Safal Investments Mauritius Limited na matawi yake (ambayo ni pamoja na Mabati Rolling Mills Limited, Kenya, na ALAF Limited, Tanzania) inajulikana kwa jina la jumla la The Safal Group. Hii ni kampuni kubwa kabisa inayotengeneza mabati katika nchi 12 za Afrika. www.safalgroup.com

 • Mabati Rolling Mills Limited (MRM) ilibuniwa zaidi ya miaka 50 iliyopita. Ni kampuni kubwa kabisa Kenya inayotengeneza mabati ya kuezekea mapaa, na inaongoza katika utanzu huu wa ufundi. Pia inaongoza katika bara la Afrika kwa kutengeneza mabati ikitumia teknolojia ya hali ya juu kabisa inayopatikana duniani. Mabati yake maarufu yanasifika na yanaaminiwa na mamilioni ya wajenzi. www.mabati.com
 • Safal MRM Foundation, yenye makao yake Kenya, ni kitengo cha Mabati Rolling Mills na Safal Group kinachoshughulika na kutoa misaada ya aina mbalimbali. Miongoni mwa misaada hiyo, inayotolewa Mariakani, Kenya, ni kuanzisha na kuendelea kugharimia uendeshaji wa Taasisi ya Mabati ya Mafunzo ya Teknolojia (Mabati Technical Training Institute), na Kituo cha Mabati cha Matibabu (Mabati Medical Centre). www.safalmrmfoundation.org
 • ALAF Limited (ALAF) ni kampuni ya Tanzania inayoongoza katika utengenezaji wa mabati ya kuezekea mapaa. Tangu ilipobuniwa mwaka 1960, ALAF imeendelea kuchangia kwa kiasi kikubwa katika shughuli za ujenzi nchini. ALAF haitengenezi mabati ya kuezekea mapaa tu, bali pia aina za nyaya za chuma zinazotumika katika ujenzi wa mapaa. ALAF pia inatengeneza mabomba ya metali yanayotumika katika shughuli mbalimbali za ufundi. www.alaf.co.tz 

Ofisi ya Makamu wa Mkuu wa Maswala ya Kimataifa katika Chuo Kikuu cha Cornell inatoa mwongozo na kusaidia katika kusimamia juhudi za kuzidisha shughuli za kimataifa Cornell. Lengo lake ni kushirikiana na shule, vyuo na taasisi nyengine ili kuendeleza na kutekeleza mipango inayohusiana na shughuli za kimataifa za Chuo Kikuu hiki. Ofisi hii inaisaidia Halmashauri mpya ya Kimataifa, ambayo mwenyekiti wake ni Makamu wa Mkuu. http://international.cornell.edu/international_vision

Idara ya Taaluma za Afrika na Utafiti inachangia kwa kiasi kikubwa katika shughuli za kitaaluma, kitamaduni na za kijamii kwenye Chuo Kikuu cha Cornell, Ithaca. http://www.asrc.cornell.edu

East African Educational Publisher (EAEP) ni shirika mojawapo kuu la wachapishaji. EAEP linajitahidi kuyahusisha maadili yanayoonekana kama kwamba yanakinzana; yaani kuchapisha kazi za kiwango cha juu zinazogusia maswala ya kijamii, ya kitamaduni na ya kiuchumi, na wakati huo huo kufaulu kufanya biashara iliyo tayari kukabiliana na hali halisi na misukosuko ya zama za kiteknolojia. http://www.eastafricanpublishers.com

Africa Poetry Book Fund inaimarisha na kuendeleza uchapishaji wa sanaa za kishairi kupitia vitabu vyake, mashindano, warsha, semina, pamoja na kushirikiana na wachapishaji, matamasha, mawakala, vyuo, vyuo vikuu, makongamano, na vikundi vingine vinavyohusika na ushairi Afrika. http://africanpoetrybf.unl.edu/

Bodi ya Wadhamini: Abdilatif Abdalla (Mwenyekiti), Mukoma wa Ngugi, Lizzy Attree, Happiness Bulugu, Walter Bgoya, Henry Chakava, Chege Githiora, Carole Boyce Davies, Rajeev Shah, na Ngugi Wa Thiong’o.

Tovuti: http://blogs.cornell.edu/kiswahiliprize/ Twitter: @KiswahiliPrize Facebook: https://www.facebook.com/pages/Mabati-Cornell-Kiswahili-Prize-for-African-Literature/1534905843433822

Mawasiliano: Prof. Mukoma Wa Ngugi, Cornell University, kiswahiliprize@cornell.edu Dr Lizzy Attree, kiswahiliprize@cornell.edu

Skip to toolbar