Home

TUZO YA KISWAHILI YA MABATI-CORNELL

YA FASIHI YA AFRIKA

Tangazo la Washindi wa 2018

Washindi wa mwaka 2018 wa Tuzo ya Kiswahili ya Mabati-Cornell ya Fasihi ya Afrika walitangazwa na Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini, Abdilatif Abdalla, leo, Januari 23, 2019.

Madhumuni makuu ya Tuzo hii, iliyoanzishwa mwaka 2014 na Dkt. Lizzy Attree  (Richmond/Goldsmith’s, Uingereza) na Dkt. Mukoma wa Ngugi (Chuo Kikuu cha Cornell, Marekani), ni kuthamini uandishi kwa lugha za Kiafrika, kuhimiza sanaa ya tafsiri baina ya lugha za Kiafrika zenyewe kwa zenyewe, na pia kutafsiri maandishi ya lugha nyengine kwa lugha za Kiafrika.

Mwaka huu, sherehe za kuwatunuku washindi tuzo zao zitafanyika Dar es Salaam, Tanzania, tarehe 15 Februari, 2019.

Washindi wenyewe ni:

  • Zainab Alwi Baharoon (Tanzania), kwa riwaya yake, Mungu Hakopeshwi, (Tuzo ya Dola 5,000 za Marekani).
  • Jacob Ngumbau Julius (Kenya) , kwa diwani yake ya mashairi, Moto wa Kifuu, (Tuzo ya Dola 5,000 za Marekani).

Washindi hawa wamepatikana kutokana na mchujo wa orodha fupi ifuatayo, iliyotangazwa kabla:

Riwaya:

  • Zainab Alwi Baharoon (Tanzania) – Mungu Hakopeshwi
  • Yasini Hamisi Shekibulah (Tanzania) – Kilinge cha Hukumu ya Dhambi
  • Zedi Rajabu (Kenya) – Makovu ya Uhai

Ushairi:

  • Jacob Ngumbau Julius (Kenya) – Moto wa Kifuu
  • Bashiru Abdallah (Tanzania) – Wino wa Dhahabu
  • Mohamed Idrisa Haji (Tanzania) – Sauti Yangu

Miswada hii imeteuliwa kutoka jumla ya miswada 116, iliyosomwa na majaji watatu: Ahmad Kipacha, Mhadhiri wa Utafiti wa Stadi ya Mawasiliano, Taasisi ya Sayansi na Teknolojia ya Nelson Mandela, Arusha, Tanzania; Nathalie Arnold Koenings, Mwanaanthropolojia na Mhadhiri wa Maandishi ya Kubuni, Chuo cha Hampshire, Massachussets, Marekani, pia ni mwandishi wa riwaya na hadithi fupi, na mfasiri wa Fasihi

ya Kiswahili na Kiingereza; na Rocha Chimerah, Profesa wa Isimu ya Kiswahili, Chuo Kikuu cha Pwani, Kilifi, Kenya, ambaye pia ni mhakiki wa Fasihi ya Kiswahili na mwandishi wa riwaya.

Kwa Wahariri:

Tuzo ya Kiswahili ya Mabati-Cornell ya Fasihi ya Kiafrika, yenye thamani ya jumla ya Dola za Marekani 15,000, hutolewa kila mwaka kwa miswada bora, au kwa vitabu vilivyochapishwa miaka miwili kabla ya mwaka wa kutolewa zawadi, katika fani za riwaya, ushairi, wasifu na riwaya za picha. Miswada inayoshinda huchapishwa na mashirika ya uchapishaji vitabu, East African Educational Publishers (EAEP), na Mkuki na Nyota Publishers. Na mswada bora wa ushairi hufasiriwa kwa Kiingereza na kuchapishwa kitabu na shirika la Africa Poetry Book Fund.

Tuzo hii inadhaminiwa na kampuni ya Mabati Rolling Mills, Kenya, na kampuni ya ALAF Limited, Tanzania (ambazo ni miongoni mwa kampuni za Safal Mauritius Limited); pia na Ofisi ya Makamu wa Mkuu wa Maswala ya Kimataifa katika Chuo Kikuu cha Cornell, na Idara ya Taaluma za Afrika ya Chuo Kikuu cha Cornell, Marekani.

Kampuni ya Safal Investments Mauritius Limited na matawi yake (ambayo ni pamoja na Mabati Rolling Mills Limited, Kenya, na ALAF Limited, Tanzania) inajulikana kwa jina la jumla la The Safal Group. Hii ni kampuni kubwa kabisa inayotengeneza mabati katika nchi 12 za Afrika. www.safalgroup.com

Mabati Rolling Mills Limited (MRM) ilibuniwa zaidi ya miaka 50 iliyopita. Ni kampuni kubwa kabisa Kenya inayotengeneza mabati ya kuezekea mapaa, na inaongoza katika utanzu huu wa ufundi. Pia inaongoza katika bara la Afrika kwa kutengeneza mabati ikitumia teknolojia ya hali ya juu kabisa inayopatikana duniani. Mabati yake maarufu yanasifika na yanaaminiwa na mamilioni ya wajenzi. www.mabati.com

Safal MRM Foundation, yenye makao yake Kenya, ni kitengo cha Mabati Rolling Mills na Safal Group kinachoshughulika na kutoa misaada ya aina mbalimbali. Miongoni mwa misaada hiyo, inayotolewa Mariakani, Kenya, ni kuanzisha na kuendelea kugharimia uendeshaji wa Taasisi ya Mabati ya Mafunzo ya Teknolojia (Mabati Technical Training Institute), na Kituo cha Mabati cha Matibabu (Mabati Medical Centre). www.safalmrmfoundation.org

ALAF Limited (ALAF) ni kampuni ya Tanzania inayoongoza katika utengenezaji wa mabati ya kuezekea mapaa. Tangu ilipobuniwa mwaka 1960, ALAF imeendelea kuchangia kwa kiasi kikubwa katika shughuli za ujenzi nchini. ALAF haitengenezi mabati ya kuezekea mapaa tu, bali pia aina za nyaya za chuma zinazotumika katika ujenzi wa mapaa. ALAF pia inatengeneza mabomba ya metali yanayotumika katika shughuli mbalimbali za ufundi. www.alaf.co.tz

Ofisi ya Makamu wa Mkuu wa Maswala ya Kimataifa katika Chuo Kikuu cha Cornell inatoa mwongozo na kusaidia katika kusimamia juhudi za kuzidisha shughuli za kimataifa Cornell. Lengo lake ni kushirikiana na shule, vyuo na taasisi nyengine ili kuendeleza na kutekeleza mipango inayohusiana na shughuli za kimataifa za Chuo Kikuu hiki. Ofisi hii inaisaidia Halmashauri mpya ya Kimataifa, ambayo mwenyekiti wake ni Makamu wa Mkuu. http://international.cornell.edu/international_vision

Idara ya Taaluma za Afrika na Utafiti inachangia kwa kiasi kikubwa katika shughuli za kitaaluma, kitamaduni na za kijamii kwenye Chuo Kikuu cha Cornell, Ithaca. http://www.asrc.cornell.edu

East African Educational Publisher (EAEP) ni shirika mojawapo kuu la wachapishaji. EAEP linajitahidi kuyahusisha maadili yanayoonekana kama kwamba yanakinzana; yaani kuchapisha kazi za kiwango cha juu zinazogusia maswala ya kijamii, ya kitamaduni na ya kiuchumi, na wakati huo huo kufaulu kufanya biashara iliyo tayari kukabiliana na hali halisi na misukosuko ya zama za kiteknolojia. http://www.eastafricanpublishers.com

Mkuki na Nyota Publishers ni shirika huru la uchapishaji vitabu vya kimaendeleo, kiukombozi, vya bei nafuu na maridadi. Shirika hili lilianzishwa mwaka 1991 kutokana na ukosefu wa vitabu vya kiwango cha juu nchini Tanzania. Kaulimbiu yake ni kuchapisha “Vitabu Vinavyofaa, Vitabu vya Bei Nafuu, na Vitabu Maridadi.” Disemba 2018 shirika hili liliichapisha diwani ya mshairi Dotto Rangimoto, Mwanangu Rudi Nyumbani, iliyoshinda nafasi ya kwanza ya ushairi katika mashindano haya ya mwaka 2017. Na mwezi wa Januari 2019 litaichapisha riwaya ya Ali Hilal Ali, Mmeza Fupa, iliyoshinda nafasi ya kwanza ya mashindano haya katika sehemu ya riwaya, mwaka 2017. http://www.mkukinanyota.com

Africa Poetry Book Fund inaimarisha na kuendeleza uchapishaji wa sanaa za kishairi kupitia vitabu vyake, mashindano, warsha, semina, pamoja na kushirikiana na wachapishaji, matamasha, mawakala, vyuo, vyuo vikuu, makongamano, na vikundi vingine vinavyohusika na ushairi Afrika. http://africanpoetrybf.unl.edu/

Bodi ya Wadhamini: Abdilatif Abdalla (Mwenyekiti), Mukoma wa Ngugi, Lizzy Attree, Happiness Bulugu, Walter Bgoya, Henry Chakava, Chege Githiora, Carole Boyce Davies, Rajeev Shah, na Ngugi Wa Thiong’o.

Majaji wa 2018

Dkt. Ahmad Kipacha alipata shahada yake ya uzamivu kuhusu lahaja za Kiswahili, Chuo Kikuu cha London (SOAS) mwaka 2005. Kabla ya hapo alihitimu shahada yake ya kwanza na ya pili katika taaluma za Kiswahili na Kiingereza, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. Hivi sasa ni Mhadhiri wa Utafiti wa Stadi ya Mawasiliano, kwenye Taasisi ya Sayansi na Teknolojia ya Nelson Mandela, Arusha, Tanzania; na pia ni Mkuu wa Idara ya Utawala, Uongozi, na Sanaa katika Skuli ya Biashara na Sanaa. Pia ni Mhadhiri Mwandamizi wa Kiswahili katika Kituo cha Maendeleo cha MS-TCDC, Arusha. Anajishugulisha na utafiti wa lugha ya Kiswahili, uhakiki wa Fasihi ya Kiswahili, na maingiliano baina ya Sanaa za Kijadi za Kiswahili na Ujasiriamali wa Kijamii.

Dkt. Nathalie Arnold Koenings ni mwandishi wa riwaya, mfasiri wa maandishi ya Fasihi ya Kiswahili na Kiingereza, na mwanaanthropolojia. Vitabu vyake viwili alivyochapisha kwa kutumia jina N.S. Koenings, ni The Blue Taxi (riwaya) na Theft (mkusanyo wa hadithi fupi) – ambavyo mazingira yake na jamii za wahusika ni za Afrika Mashariki, alikokulia. Hadithi zake nyengine zimechapishwa katika majarida Story Quarterly, Glimmer Train, na The Enkare Review. Miongoni mwa tafsiri zake za Kiingereza kutoka Kiswahili ni za maandishi ya Mwenda Mbatiah, Mohammed Said Abdulla, na A.S. Manyanza, zilizochapishwa katika majarida ya New Orleans Review, Words without Borders, na Asymptote. Tafsiri yake ya Kiswahili ya hadithi fupi ya Kiingereza ‘Genesis’ (au ‘Mwanzo’), iliyotungwa na Tope Folarin, ilikuwa ni sehemu ya mradi wa tafsiri wa Kiswahili wa Tuzo ya Caine ya Maandishi ya Kiafrika. Katika fani ya anthropolojia, maandishi yake, yaliyochapishwa katika majarida Swahili Forum, Research in African Literatures, na kwengineko, yanahusu historia-simulizi na kumbukumbu na jiografia ya kijamii ya Zanzibar, hasa kisiwa cha Pemba. Nathalie anafundisha Maandishi ya Kubuni na anthropolojia katika Chuo cha Hampshire, kilichoko Massachusetts, Marekani.

Prof. Rocha Chimerah ni Profesa wa Isimu ya Kiswahili katika Chuo Kikuu cha Pwani, Kilifi, Kenya. Alihitimu shahada yake ya uzamivu mwaka 1989, Chuo Kikuu cha Ohio, Marekani. Alisomesha Rwanda kwa miaka minane, na amechapisha makala kadha wa kadha kuhusu Lugha na Fasihi ya Kiswahili katika majarida ya kitaaluma ya Afrika Mashariki na ya nchi za nje. Miongoni mwa riwaya zake zilizochapishwa ni Nyongo Mkalia Ini na Siri Sirini (juzuu tatu), kadhalika na tamthilia. Mwaka 2000 alitunukiwa Tuzo ya Noma kwa kitabu alichoshiriki kukiandika, Ufundishaji wa Fasihi: Nadharia na Mbinu. Kitabu chake kingine, Kiswahili: Past, Present and Future Horizon kiliorodheshwa na Tamasha la Vitabu, Harare, Zimbabwe, mwaka 2002 kuwa ni miongoni mwa Vitabu Bora 100 vya Afrika vya Karne ya 20.

Tovuti: http://blogs.cornell.edu/kiswahiliprize/ 
Twitter:
@KiswahiliPrize
Facebook: https://www.facebook.com/pages/Mabati-Cornell-Kiswahili-Prize for

African-Literature/1534905843433822 

Mawasiliano: Prof. Mukoma Wa Ngugi, Cornell University, kiswahiliprize@cornell.edu
Dr Lizzy Attree, kiswahiliprize@cornell.edu

Skip to toolbar