Waamuzi

Majaji wa 2018

Dkt. Ahmad Kipacha alipata shahada yake ya uzamivu kuhusu lahaja za Kiswahili, Chuo Kikuu cha London (SOAS) mwaka 2005. Kabla ya hapo alihitimu shahada yake ya kwanza na ya pili katika taaluma za Kiswahili na Kiingereza, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. Hivi sasa ni Mhadhiri wa Utafiti wa Stadi ya Mawasiliano, kwenye Taasisi ya Sayansi na Teknolojia ya Nelson Mandela, Arusha, Tanzania; na pia ni Mkuu wa Idara ya Utawala, Uongozi, na Sanaa katika Skuli ya Biashara na Sanaa. Pia ni Mhadhiri Mwandamizi wa Kiswahili katika Kituo cha Maendeleo cha MS-TCDC, Arusha. Anajishugulisha na utafiti  wa lugha ya Kiswahili, uhakiki wa Fasihi ya Kiswahili, na maingiliano baina ya Sanaa za Kijadi za Kiswahili na Ujasiriamali wa Kijamii.

 

Dkt. Nathalie Arnold Koenings ni mwandishi wa riwaya, mfasiri wa maandishi ya Fasihi ya Kiswahili na Kiingereza, na mwanaanthropolojia. Vitabu vyake viwili alivyochapisha kwa kutumia jina N.S. Koenings, ni The Blue Taxi (riwaya) na Theft (mkusanyo wa hadithi fupi) – ambavyo mazingira yake na jamii za wahusika ni za Afrika Mashariki, alikokulia. Hadithi zake nyengine zimechapishwa katika majarida Story Quarterly, Glimmer Train, na The Enkare Review. Miongoni mwa tafsiri zake za Kiingereza kutoka Kiswahili ni za maandishi ya Mwenda Mbatiah, Mohammed Said Abdulla, na A.S. Manyanza, zilizochapishwa katika majarida ya New Orleans Review, Words without Borders, na Asymptote. Tafsiri yake ya Kiswahili ya hadithi fupi ya Kiingereza ‘Genesis’ (au ‘Mwanzo’), iliyotungwa na Tope Folarin, ilikuwa ni sehemu ya mradi wa tafsiri wa Kiswahili wa Tuzo ya Caine ya Maandishi ya Kiafrika. Katika fani ya anthropolojia, maandishi yake, yaliyochapishwa katika majarida Swahili Forum, Research in African Literatures, na kwengineko, yanahusu historia-simulizi na kumbukumbu na jiografia ya kijamii ya Zanzibar, hasa kisiwa cha Pemba. Nathalie anafundisha Maandishi ya Kubuni na anthropolojia katika Chuo cha Hampshire, kilichoko Massachusetts, Marekani.

 

Prof. Rocha Chimerah ni Profesa wa Isimu ya Kiswahili katika Chuo Kikuu cha Pwani, Kilifi, Kenya. Alihitimu shahada yake ya uzamivu mwaka 1989, Chuo Kikuu cha Ohio, Marekani. Alisomesha Rwanda kwa miaka minane, na amechapisha makala kadha wa kadha kuhusu Lugha na Fasihi ya Kiswahili katika majarida ya kitaaluma ya Afrika Mashariki na ya nchi za nje. Miongoni mwa riwaya zake zilizochapishwa ni Nyongo Mkalia Ini na Siri Sirini (juzuu tatu), kadhalika na tamthilia. Mwaka 2000 alitunukiwa Tuzo ya Noma kwa kitabu alichoshiriki kukiandika, Ufundishaji wa Fasihi: Nadharia na Mbinu. Kitabu chake kingine,  Kiswahili: Past, Present and Future Horizon kiliorodheshwa na Tamasha la Vitabu, Harare, Zimbabwe, mwaka 2002 kuwa ni miongoni mwa Vitabu Bora 100 vya Afrika vya Karne ya 20.

 

Skip to toolbar