2019 Utaratibu wa Kushiriki

TUZO YA KISWAHILI YA MABATI-CORNELL

YA FASIHI YA AFRIKA: 2019

Utaratibu wa Kushiriki

  

Tunafurahi kuwajulisha utaratibu wa kushiriki katika mashindano ya Tuzo ya Kiswahili ya Mabati-Cornell ya Fasihi ya Afrika yanayoingia mwaka wake wa tano. Tuzo hii, iliyoanzishwa mwaka wa 2014 na Dkt. Lizzy Attree (Richmond/Goldsmith’s) na Dkt. Mukoma wa Ngugi (Chuo Kikuu cha Cornell, Marekani), ina madhumuni ya kutambua uandishi kwa lugha za Kiafrika, na kuhimiza sanaa ya tafsiri kutoka lugha za Kiafrika, baina ya lugha za Kiafrika, na kwa lugha za Kiafrika.

Tuzo itatolewa kwa mswada bora ambao haujachapishwa, au kitabu kilichochapishwa katika miaka miwili kabla ya mwaka wa Tuzo katika tanzu za riwaya, ushairi, mkusanyo wa hadithi fupi, tamthilia riwaya za picha na wasifu. Jumla ya $15,000 (za Marekani) zitagawanywa ifuatavyo:

Mshindi wa Kwanza (riwaya)  – $5,000

Mshindi wa Kwanza (ushairi)  – $5,000

Mshindi wa Pili (katika utanzu wowote)  – $3,000

Mshindi wa Tatu (katika utanzu wowote) – $2,000

Mswada utakaoshinda utachapishwa kwa Kiswahili na mashirika ya uchapishaji ya Mkuki na Nyota Publishers  (Tanzania) na East African Educational Publishers (Kenya). Na diwani bora itatafsiriwa kwa Kiingereza na kuchapishwa na Africa Poetry Book Fund. Sherehe ya kuwatuza washindi, itakayohudhuriwa na washindi wenyewe, itakuwa AfriKa Mashariki.

Maagizo ya Kuyapeleka Maandishi

Tafadhali peleka mswada wako au kitabu chako, klichochapishwa katika miaka miwili kabla mwaka wa Tuzo, kwa: kiswahiliprize@cornell.edu kabla ya Agosti 5, 2019.

 

Mwandishi mmoja anaweza kupeleka mswada mmoja tu au kitabu kimoja tu kila mwaka.

  • Mswada wa riwaya usipungue  maneno 50,000  na  wa ushairi usipungue kurasa 60.
  • Maandishi yote lazima yawe kwa Kiswahili
  • Mswada unaweza kupelekwa kama faili ya Microsoft Word au Rich Text. Jina la mswada liwe jina la faili.
  • Ukurasa wa kwanza wa mswada uwe na  jina la mswada, na hesabu ya maneno.
  • Mswada uchapishwe kwa mtindo wa Times New Roman, ukubwa wa pointi 12 na nafasi kati ya mistari ya 1.5.
  • Mswada uambatishwe katika baruapepe.
  • Baruapepe iwe na maelezo yafuatayo: Jina rasmi,  jina la lakabu, nambari ya simu, tawasifu fupi, tarehe ya kuzaliwa, na nchi ya kuzaliwa na ya makazi
  • Kwa vitabu vilivyochapishwa, tafadhali mwelekeze mchapishaji wako apeleke nakala tatu kwa Africana Studies and Research Center, 310 Triphammer Road, Ithaca, NY 14850, USA.

Kwa Wahariri: 

Tuzo ya Kiswahili ya Mabati-Cornell ya Fasihi ya Kiafrika, yenye thamani ya jumla ya Dola za Marekani 15,000, hutolewa kila mwaka kwa miswada bora, au kwa vitabu vilivyochapishwa miaka miwili kabla ya mwaka wa kutolewa zawadi, katika fani za riwaya, ushairi, wasifu, tamthilia na riwaya za picha. Miswada inayoshinda huchapishwa na mashirika ya uchapishaji vitabu, Mkuki na Nyota Publishers na East African Educational Publishers (EAEP). Na mswada bora wa ushairi hufasiriwa kwa Kiingereza na kuchapishwa kitabu na shirika la Africa Poetry Book Fund.

Tuzo hii inadhaminiwa na kampuni ya Mabati Rolling Mills, Kenya, na kampuni ya ALAF Limited, Tanzania (ambazo ni miongoni mwa kampuni za Safal Mauritius Limited); pia na Ofisi ya Makamu wa Mkuu wa Maswala ya Kimataifa katika Chuo Kikuu cha Cornell, Idara ya Taaluma za Afrika ya Chuo Kikuu cha Cornell, Marekani, na Wakfu wa Ngugi wa Thiong’o (Ngugi wa Thiong’o Foundation).

Kampuni ya Safal Investments Mauritius Limited na matawi yake (ambayo ni pamoja na Mabati Rolling Mills Limited, Kenya, na ALAF Limited, Tanzania) inajulikana kwa jina la jumla la The Safal Group. Hii ni kampuni kubwa kabisa inayotengeneza mabati katika nchi 12 za Afrika. www.safalgroup.com

Mabati Rolling Mills Limited (MRM) ilibuniwa zaidi ya miaka 50 iliyopita. Ni kampuni kubwa kabisa Kenya inayotengeneza mabati ya kuezekea mapaa, na inaongoza katika utanzu huu wa ufundi. Pia inaongoza katika bara la Afrika kwa kutengeneza mabati ikitumia teknolojia ya hali ya juu kabisa inayopatikana duniani. Mabati yake maarufu yanasifika na yanaaminiwa na mamilioni ya wajenzi. www.mabati.com

Safal MRM Foundation, yenye makao yake Kenya, ni kitengo cha Mabati Rolling Mills na Safal Group kinachoshughulika na kutoa misaada ya aina mbalimbali. Miongoni mwa misaada hiyo, inayotolewa Mariakani, Kenya, ni kuanzisha na kuendelea kugharimia uendeshaji wa Taasisi ya Mabati ya Mafunzo ya Teknolojia (Mabati Technical Training Institute), na Kituo cha Mabati cha Matibabu (Mabati Medical Centre). www.safalmrmfoundation.org

ALAF Limited (ALAF) ni kampuni ya Tanzania inayoongoza katika utengenezaji wa mabati ya kuezekea mapaa. Tangu ilipobuniwa mwaka 1960, ALAF imeendelea kuchangia kwa kiasi kikubwa katika shughuli za ujenzi nchini. ALAF haitengenezi mabati ya kuezekea mapaa tu, bali pia aina za nyaya za chuma zinazotumika katika ujenzi wa mapaa. ALAF pia inatengeneza mabomba ya metali yanayotumika katika shughuli mbalimbali za ufundi. www.alaf.co.tz

Ofisi ya Makamu wa Mkuu wa Maswala ya Kimataifa katika Chuo Kikuu cha Cornell inatoa mwongozo na kusaidia katika kusimamia juhudi za kuzidisha shughuli za kimataifa Cornell. Lengo lake ni kushirikiana na shule, vyuo na taasisi nyengine ili kuendeleza na kutekeleza mipango inayohusiana na shughuli za kimataifa za Chuo Kikuu hiki. Ofisi hii inaisaidia Halmashauri mpya ya Kimataifa, ambayo mwenyekiti wake ni Makamu wa Mkuu. http://international.cornell.edu/international_vision

Idara ya Taaluma za Afrika na Utafiti inachangia kwa kiasi kikubwa katika shughuli za kitaaluma, kitamaduni na za kijamii kwenye Chuo Kikuu cha Cornell, Ithaca. http://www.asrc.cornell.edu

Ngugi Wa Thiong’o Foundation Wakfu huu unapata nguvu zake kutokana na hamu  na ari ya kukuza kuonekana kwa Lugha za Kiafrika nchini Kenya, barani Afrika, na duniani, na kutambuliwa kuwa ni vyombo mwafaka vya kuendeshea shughuli za sanaa ya uigizaji, ubunifu, uvumbuzi, na taaluma. Pia unazitambua lugha hizi kwamba zina uwezo wa kuwa mstari wa mbele katika kila fani – tangu utamaduni, sayansi za kibiolojia, teknolojia hadi tiba.   http://ngugiwathiongofoundation.org

East African Educational Publisher (EAEP) ni shirika mojawapo kuu la wachapishaji. EAEP linajitahidi kuyahusisha maadili yanayoonekana kama kwamba yanakinzana; yaani kuchapisha kazi za kiwango cha juu zinazogusia maswala ya kijamii, ya kitamaduni na ya kiuchumi, na wakati huo huo kufaulu kufanya biashara iliyo tayari kukabiliana na hali halisi na misukosuko ya zama za kiteknolojia. http://www.eastafricanpublishers.com

Mkuki na Nyota Publishers ni shirika huru la uchapishaji vitabu vya kimaendeleo, kiukombozi, vya bei nafuu na maridadi. Shirika hili lilianzishwa mwaka 1991 kutokana na ukosefu wa vitabu vya kiwango cha juu nchini Tanzania. Kaulimbiu yake ni kuchapisha “Vitabu Vinavyofaa, Vitabu vya Bei Nafuu, na Vitabu Maridadi.” Disemba 2018 shirika hili liliichapisha diwani ya mshairi Dotto Rangimoto, Mwanangu Rudi Nyumbani, iliyoshinda nafasi ya kwanza ya ushairi katika mashindano haya ya mwaka 2017. Na mwezi wa Januari 2019 likaichapisha riwaya ya Ali Hilal Ali, Mmeza Fupa, iliyoshinda nafasi ya kwanza ya mashindano haya katika sehemu ya riwaya, mwaka 2017. http://www.mkukinanyota.com

Africa Poetry Book Fund inaimarisha na kuendeleza uchapishaji wa sanaa za kishairi kupitia vitabu vyake, mashindano, warsha, semina, pamoja na kushirikiana na wachapishaji, matamasha, mawakala, vyuo, vyuo vikuu, makongamano, na vikundi vingine vinavyohusika na ushairi Afrika. http://africanpoetrybf.unl.edu/

Bodi ya Wadhamini: Abdilatif Abdalla (Mwenyekiti), Mukoma wa Ngugi, Lizzy Attree, Happiness Bulugu, Walter Bgoya, Henry Chakava, Chege Githiora, Carole Boyce Davies, Rajeev Shah, na Ngugi Wa Thiong’o.

Skip to toolbar