TUZO YA KISWAHILI YA MABATI-CORNELL YA FASIHI YA AFRIKA
Inayoungwa mkono na Kampuni ya ALAF Li

Washindi wa mwaka 2016 wa Tuzo ya Kiswahili ya Mabati-Cornell ya Fasihi ya Afrika walitangazwa na Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini, Abdilatif Abdalla, tarehe 14 Disemba, 2016.

Madhumuni makuu ya Tuzo hii, iliyoanzishwa mwaka 2014 na Dkt. Lizzy Attree (Mkurugenzi wa Tuzo ya Caine) na Dkt. Mukoma wa Ngugi (Chuo Kikuu cha Cornell, Marekani), ni kuthamini uandishi kwa lugha za Kiafrika, kuhimiza sanaa ya tafsiri baina ya lugha za Kiafrika zenyewe kwa zenyewe, na pia kutafsiri maandishi ya lugha nyengine kwa lugha za Kiafrika.

Washindi wa mwaka 2016 ni:

Riwaya

1. Idrissa Haji Abdalla (Tanzania), Kilio cha Mwanamke ($5,000)

idrissa-bw Idrissa Haji Abdalla alizaliwa katika kijiji cha Uroa, Zanzibar, Tanzania. Alianza kufanya kazi Idara ya Polisi, Tanzania, mwaka 1989, kwenye kituo cha Pemba Kaskazini.

Mwaka 1998 alikata shauri kuendelea na masomo kwenye Taasisi ya Kiswahili na Lugha za Kigeni (TAKILUKI), ambako alifaulu mtihani wa Kidato cha Nne. Aliendelea na masomo ya Kidato cha Tano kwenye Shule ya Sekondari ya Lumumba, Zanzibar, ambako alihitimu na kufaulu mtihani wa Kidato cha Sita mwaka 2001.

Alianza sanaa ya kutunga mashairi alipokuwa katika mwaka wa pili wa masomo ya sekondari. Baadaye, alipokuwa akifanya kazi Pemba, alianza kuandika hadithi fupi fupi na tamthilia. Baadhi kubwa ya mashairi na hadithi zake zilichapishwa katika magazeti ya Tanzania, na pia kusomwa kwenye kituo cha redio cha Sauti ya Tanzania, Zanzibar.

Ana miswada miwili ambayo bado haijachapishwa vitabu: Dhambi ya Ubinafsi (riwaya), na Saa ya  Mabadiliko (mashairi).

Anaendelea kufanya kazi Idara ya Polisi, Tanzania. Ameoa na ana watoto watatu.

2. Hussein Wamaywa (Tanzania), Moyo Wangu Unaungua ($3,000)

hussein-wamaywa-bw Hussein Wamaywa alizaliwa Ujiji, Tanzania, mwaka 1980. Baada ya masomo ya shule ya sekondari, mwaka 2004 alipata stishihada ya kozi ya Jinsia na Maendeleo katika kituo cha Tanzania Gender and Networking Programme.

Mwaka 2007 alipata Diploma katika shughuli za utengenezaji na uongozaji filamu kwenye Chuo cha Dhahabu cha Sanaa ya Filamu baada ya mafunzo ya miaka miwili. Pia alishiriki katika kozi fupi Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kuhusu uandishi wa kazi za ubunifu. Ana stishihada ya Uandishi wa Habari kutoka Royal College of Tanzania.

Tangu miaka kumi iliyopita, Hussein Wamaywa amekuwa akifanya kazi kwenye magazeti mbalimbali. Hivi sasa anayafanyia kazi magazeti ya Sani na Raia Tanzania. Yeye pia ni mwanaharakati wa haki za kibinadamu, usawa wa jinsia na maendeleo; pamoja na kuwa ni mkufunzi wa mafunzo ya maendeleo endelevu

Huu ukiwa upande mmoja, upande wa pili Wamaywa ni mwanaharakati wa Haki za Binadamu, Jinsia na Maendeleo na Mwezeshaji ngazi ya Jamii na amefanya kazi na Mashirika mbalimbali ya ndani na nje ya nchi katika kupigania maendeleo endelevu kwa walio masikini na wanaoishi vijijini.

Hussein ni Afisa Mipango wa shirika lisilo la serikali, Mpakani Tunaweza.

Ushairi

1. Ahmed Hussein Ahmed (Kenya), Haile Ngoma ya Wana ($5,000)

a-h-a-bwAhmed Hussein Ahmed ana shahada ya BA kutoka Chuo Kikuu cha Kenyatta, Nairobi; na pia Diploma ya Lugha ya Kiarabu, na shahada ya Uzamili (MA), kutoka Chuo Kikuu cha Sokoto, Nigeria. Ni Mhadhiri katika Chuo Kikuu cha Pwani, Kilifi, Kenya.

Mwaka 2012 alitunukiwa Tuzo ya Mshairi Bora, kutoka Taasisi ya Taaluma za Kiswahili Afrika ya Mashairiki (RISSEA), Mombasa.

Mwaka 2010 alichapisha diwani yake ya kwanza, Mashairi Bulbul (Oxford University Press, Nairobi). Alishirikiana na washairi wengine katika diwani ya Sauti ya Shangwe, waliyoichapisha wenyewe mwaka 2011. Mwaka 2012 alihariri na kuchapisha Ambari, diwani ya mashairi ya washairi mbalimbali.

Hadithi zake fupi fupi, Kesho! Kesho! (2009), Mgeni Njoo! (2009) na Kifimbo Cheza (2003) zilichapishwa pia na shirika la Oxford University Press, Nairobi.

Hivi sasa ni mwanafunzi wa Shahada ya Uzamifu (PhD), na pia Mtafiti katika Kituo cha Taaluma ya Utamaduni wa Miswada, Chuo Kikuu cha Hamburg, Ujerumani.


Kama ilivyotangazwa kabla, wafuatao ni waandishi wengine waliokuwamo katika orodha fupi:

  • Ally Hilal (Tanzania), Mmeza Fupa (riwaya)
  • Hussein Wamaywa (Tanzania), Mkakati wa Kuelekea Ikulu (riwaya)
  • Richard Atuti Nyabuya (Kenya), Umalenga wa Nyanda za Juu (ushairi)

Maandishi hayo ni miongoni mwa miswada 20 iliyosomwa na waamuzi watatu:

  • Prof. Rayya Timammy – Profesa Mshiriki, Idara ya Kiswahili, Chuo Kikuu cha Nairobi
  • Dkt. Shani Omari – Mhadhiri Mwandamizi, Idara ya Fasihi, Mawasiliano na Uchapishaji, Taasisi ya Taaluma za Kiswahili, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam
  • Prof. Joshua S. Madumulla – Profesa Mshiriki wa Fasihi, Chuo Kikuu cha Tumaini, Iringa

Wakizingatia historia ndefu ya fasihi ya Kiswahili, waamuzi walisema, “Kwenye riwaya iliyopata ushindi wa kwanza, swala la mwanamke limejadiliwa kwa urefu. Mwanamke amewakilishwa katika nyanja na nafasi zake mbalimbali katika jamii. Mila na desturi zinazotumiwa kumkandamiza mwanamke zimedhihirishwa kuwa ni miongoni mwa vikwazo vikubwa vinavyomzuia mwanamke kuendelea na kufanikiwa. Lakini mwanamke anapambana dhidi ya vikwazo hivyo na, hatimaye, anafaulu.”

Mashairi yaliyomo katika muswada ulioshinda yametungwa kwa lahaja ya Kimvita, inayozungumzwa Mombasa. Lahaja hii imetumiwa na washairi maarufu wa nyakati mbalimbali katika historia; kwa mfano Muyaka wa Muhaji, mshairi mashuhuri wa karne ya 19. Pia imetumiwa na washairi wa wakati wetu huu: Ahmad Nassir Juma Bhalo, Abdilatif Abdalla, na sasa Ahmed Hussein Ahmed. Hii ni lahaja iliyo na utajiri mkubwa wa msamiati  na sauti mbalimbali za matamshi ya maneno.”

Mwaka huu, zawadi za Tuzo hii zitatolewa Tanzania katika Hoteli ya Hyatt Regency Dar es Salaam, Kilimanjaro, Ukumbi wa Kibo, tarehe 16 Januari, 2017.

Kwa Wahariri:

Tuzo ya Kiswahili ya Mabati-Cornell ya Fasihi ya Kiafrika, yenye thamani ya jumla ya Dola za Marekani 15,000, hutolewa kila mwaka kwa miswada bora, au kwa vitabu vilivyochapishwa miaka miwili kabla ya mwaka wa kutolewa zawadi, katika fani za riwaya, ushairi, wasifu na riwaya za picha. Miswada inayoshinda huchapishwa na shirika la uchapishaji vitabu la East African Educational Publishers (EAEP). Na mswada bora wa ushairi hufasiriwa kwa Kiingereza na kuchapishwa kitabu na shirika la Africa Poetry Book Fund.

Tuzo hii inadhaminiwa na kampuni ya Mabati Rolling Mills, Kenya, na kampuni ya ALAF Limited, Tanzania (ambazo ni miongoni mwa kampuni za Safal Mauritius Limited); pia na Ofisi ya Makamu wa Mkuu wa Maswala ya Kimataifa katika Chuo Kikuu cha Cornell, na Idara ya Taaluma za Afrika ya Chuo Kikuu cha Cornell, Marekani.

Kampuni ya Safal Investments Mauritius Limited na matawi yake (ambayo ni pamoja na Mabati Rolling Mills Limited, Kenya, na ALAF Limited, Tanzania) inajulikana kwa jina la jumla la The Safal Group. Hii ni kampuni kubwa kabisa inayotengeneza mabati katika nchi 12 za Afrika. www.safalgroup.com

  • Mabati Rolling Mills Limited (MRM) ilibuniwa zaidi ya miaka 50 iliyopita. Ni kampuni kubwa kabisa Kenya inayotengeneza mabati ya kuezekea mapaa, na inaongoza katika utanzu huu wa ufundi. Pia inaongoza katika bara la Afrika kwa kutengeneza mabati ikitumia teknolojia ya hali ya juu kabisa inayopatikana duniani. Mabati yake maarufu yanasifika na yanaaminiwa na mamilioni ya wajenzi. www.mabati.com
  • Safal MRM Foundation, yenye makao yake Kenya, ni kitengo cha Mabati Rolling Mills na Safal Group kinachoshughulika na kutoa misaada ya aina mbalimbali. Miongoni mwa misaada hiyo, inayotolewa Mariakani, Kenya, ni kuanzisha na kuendelea kugharimia uendeshaji wa Taasisi ya Mabati ya Mafunzo ya Teknolojia (Mabati Technical Training Institute), na Kituo cha Mabati cha Matibabu (Mabati Medical Centre). www.safalmrmfoundation.org
  • ALAF Limited (ALAF) ni kampuni ya Tanzania inayoongoza katika utengenezaji wa mabati ya kuezekea mapaa. Tangu ilipobuniwa mwaka 1960, ALAF imeendelea kuchangia kwa kiasi kikubwa katika shughuli za ujenzi nchini. ALAF haitengenezi mabati ya kuezekea mapaa tu, bali pia aina za nyaya za chuma zinazotumika katika ujenzi wa mapaa. ALAF pia inatengeneza mabomba ya metali yanayotumika katika shughuli mbalimbali za ufundi. www.alaf.co.tz 

Ofisi ya Makamu wa Mkuu wa Maswala ya Kimataifa katika Chuo Kikuu cha Cornell inatoa mwongozo na kusaidia katika kusimamia juhudi za kuzidisha shughuli za kimataifa Cornell. Lengo lake ni kushirikiana na shule, vyuo na taasisi nyengine ili kuendeleza na kutekeleza mipango inayohusiana na shughuli za kimataifa za Chuo Kikuu hiki. Ofisi hii inaisaidia Halmashauri mpya ya Kimataifa, ambayo mwenyekiti wake ni Makamu wa Mkuu. http://international.cornell.edu/international_vision

Idara ya Taaluma za Afrika na Utafiti inachangia kwa kiasi kikubwa katika shughuli za kitaaluma, kitamaduni na za kijamii kwenye Chuo Kikuu cha Cornell, Ithaca. http://www.asrc.cornell.edu

East African Educational Publisher (EAEP) ni shirika mojawapo kuu la wachapishaji. EAEP linajitahidi kuyahusisha maadili yanayoonekana kama kwamba yanakinzana; yaani kuchapisha kazi za kiwango cha juu zinazogusia maswala ya kijamii, ya kitamaduni na ya kiuchumi, na wakati huo huo kufaulu kufanya biashara iliyo tayari kukabiliana na hali halisi na misukosuko ya zama za kiteknolojia. http://www.eastafricanpublishers.com

Africa Poetry Book Fund inaimarisha na kuendeleza uchapishaji wa sanaa za kishairi kupitia vitabu vyake, mashindano, warsha, semina, pamoja na kushirikiana na wachapishaji, matamasha, mawakala, vyuo, vyuo vikuu, makongamano, na vikundi vingine vinavyohusika na ushairi Afrika. http://africanpoetrybf.unl.edu/

Bodi ya Wadhamini: Abdilatif Abdalla (Mwenyekiti), Mukoma wa Ngugi, Lizzy Attree, Happiness Bulugu, Walter Bgoya, Henry Chakava, Chege Githiora, Carole Boyce Davies, Rajeev Shah, na Ngugi Wa Thiong’o.

Tovuti: http://blogs.cornell.edu/kiswahiliprize/
Twitter: @KiswahiliPrize
Facebook: https://www.facebook.com/pages/Mabati-Cornell-Kiswahili-Prize-for-African-Literature/1534905843433822

Mawasiliano:
Prof. Mukoma Wa Ngugi, Cornell University, kiswahiliprize@cornell.edu
Dr Lizzy Attree, kiswahiliprize@cornell.edu

Speak Your Mind

*

Skip to toolbar